Sibuka FM

Bariadi DC yatoa mikopo ya zaidi milioni 250,Simalenga amesema siyo mgao

28 November 2026, 05:49

Pichani ni mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Simon Simalenga akizungumza jambo na wanufaikaji wa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani katika halmashauri hiyo waliopata mikopo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi Picha kutoka ofisi ya DC Bariadi

“Tunataka kuona watu wanapata manufaa kutokana na mikopo ya asilimia kumi isiyo na riba itakuwa ni masikitiko makubwa sana kama kuna watu wanachukua mikopo hii kwa ajili ya kufanya starehe badala ya kufanya shughuli za uchumi”. 

Na,Daniel Manyanga 

Mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu,Simon Simalenga amewataka wale wote waliopatiwa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya ya Bariadi, kuhakikisha wanazirejesha fedha hizo ili kuwapa fursa na watu wengine kukopeshwa na kunufaika nazo ili kuongeza thamani katika shughuli za kiuchumi wanazozifanya.

Picha ya pamoja ikimuonesha mkuu wa wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga akikabidhi mfano wa hundi kwa vikundi vya vijana,wanawake na watu wenye ulemavu waliopata mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri Picha kutoka ofisi ya DC Bariadi

Akizungumza wakati wa kukabidhi mikopo hiyo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika halmashauri hiyo, mkuu huyo wa wilaya ya Bariadi amesema kuwa ni muhimu wanaokopa fedha hizo kuhakikisha wanazirejesha ili kuwanufaisha na watu wengine pia huku akipongeza vikundi vilivyorejesha mikopo.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga

Mayala Lucas ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi, amesema kuwa halmashauri hiyo itaendelea kusimamia ili kuhakikisha fedha hizo za mikopo zinaendelea kutengwa, huku mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Bariadi,Tinana Masanja akisema kuwa atashirikiana na halmashauri kuhakikisha vijana wote waliokopeshwa wanarejesha mikopo hiyo.

Sauti ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi na UVCCM wilaya hiyo

Awali akitoa taarifa ya mikopo hiyo iliyotolewa na halmashauri hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 kaimu afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri hiyo Zakia Boniphace, ametaja kiasi cha fedha kilichotolewa, huku wanufaika wa mikopo hiyo wakikisitiza kuchukuliwa hatua wale wote watakaoshindwa kuirejesha mikopo kwa wakati ili kuwawezesha na wengine kunufaika na mikopo hiyo.

Sauti ya kaimu afisa maendeleo ya jamii na wanufaikaji wa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri
Pichani ni baadhi ya wanufaikaji wa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani Picha kutoka ofisi ya DC Bariadi