Sibuka FM

22 wafariki kwa kuporomokewa na kifusi mgodini Simiyu

14 January 2024, 12:42 pm

Pichani ni Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Simiyu INS.Faustine Mtitu akizungumza na waandishi wa habari akiwa eneo la tukio lilipotea tukio la vifo 22 vya wachimbaji wadogo wa madini katika mgodi wa Dhahabu wa Ikinabushu Picha na Daniel Manyanga

Tumefanikiwa kuokoa miili ishirini na mbili ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Ikinabushu kufuatia kuporomoka kwa duara wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji

Na,Daniel Manyanga

Watu ishirini na mbili  wamefariki dunia  kwa kufukiwa  (kuporomokewa) na kifusi kwenye machimbo ya madini ya dhahabu yaliyopo katika kijiji cha Ikinabushu kata ya Gilya wilayani Bariadi mkaoni Simiyu wakiwa ndani ya duara.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Simiyu INSP.Faustine Mtitu akiwa  eneo la tukio  amesema kuwa tukio hilo limetokea mnamo tarehe 13.01.2024 majira ya saa kumi na moja alfajiri katika mgodi huo wa Ikinabushu uliopo kata ya Gilya huku chanzo  cha vifo hivyo kikiwa ni ardhi kuporomoka  kutokana na kulowana kufuatia  mvua  kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani hapo.

INSP.Mtitu ameongeza kuwa zoezi la uokoaji kupitia jeshi la Zimamoto la uokoaji kwa ushirikiano na Wachimbaji wadogo mgodini hapo lilianza mara moja baada ya kupata taarifa  ambapo hadi wanasitisha zoezi la uokoaji mnamo majira ya saa mbili na nusu usiku walifanikiwa kutoa miili 22 ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu na yote ni ya kiume.

“Wachimbaji waliingia kwenyea duara bila kufuata utaratibu wa migodini maana kila mchimbaji anapoingia kwenye duara lazima aweze kujiorodhesha kwenye daftari ili kuwa rahisi kujuwa ameingia muda gani maana kwenye duara kuna oksijeni ndogo”Amesema Mtitu

“Mpaka majira ya saa mbili na nusu usiku ambapo zoezi tunalisitisha tulifanikiwa kuokoa miili 22 hivyo leo tumekuja kuhakiki kama kuna miili mingine ambayo ilibakia lakini hakuna hata mwili mmoja na kubaki idadi ile ile hivyo niwapongeze sana Waandishi wa habari kwa kuendelea kuujuza umma juu ya tukio hili bila kusahau Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Wachimbaji wadogo kwa kuweza kufanikisha zoezi zima kuanzia jana”Amesema Mtitu

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda ,amesema kuwa tukio hilo ni la kwanza kutokea mkoani hapo kuua watu wengi kiasi hicho na kuacha simanzi kubwa kwa wahanga ambapo kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapo imesitisha shughuli za uchimbaji katika mgodi huo mpaka pale watakapojiridhisha kama ni salama kwa wachimbaji kuendelea na  shughuli hizo.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda akizungumzia swala la kufungwa kwa shughuli za uchimbaji katika mgodi huo kutokana na watu 22 kufariki wakiwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji usiku wa manane

Taarifa za awali kutoka kwa wasimamizi wa mgodi huo zimeeleza kuwa  shughuli za uchumbaji zilisitishwa kutokana na kupewa ushauri  kutoka kwa wakaguzi wa mgodi huo  lakini  baadhi ya wachimbaji  walikaadi agizo hilo na kuingia kinyemera na kuanza kuchimba mnano majira ya usiku wa manane.

Sauti za wasimamizi wa mgodi huo wakizungumza na Waandishi wa habari namna ambavyo tukio lilivyotokea na kusababisha maafa hayo
Picha katika matukio mbalimbali zikionesha namna jinsi ambavyo tukio la uokozi likiendelea katika mgodi wa dhahabu wa Ikinabushu kufuatia wachimbaji wadogo 22 kufariki dunia wakati wakiendelea na uchimbaji.