Sibuka FM

Itilima:Jela miaka 30 kwa Kubaka,Kumtorosha na Kumshawishi kumuoa mwanafunzi

8 August 2023, 7:24 pm

Pichani:Mahakama ya wilaya ya Itilima ambapo hukumu ya Masunga imesomwa: Picha na Daniel Manyanga

Mahakama ya wilaya ya Itilima imemuhukumu ,Malimi Masunga kwenda jela miaka 30 kwa makosa matatu,Kubaka ,Kumtorosha na kumshawishi kumuoa mwanafunzi chini ya miaka 16.

Na,Daniel Manyanga

Mahakama ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Malimi Masunga(24) mkazi wa Mwamugesha kwa makosa matatu,Kumtorosha Mwanafunzi chini ya miaka 16,Kubaka na Kushawishi kumuoa mwanafunzi  chini ya miaka 16 hukumu iliyosomwa tarehe 07/08/2023.

Kwa mujibu wa mkaguzi msaidizi wa polisi Jaston Mhule amedai kuwa mnamo tarehe 14/06/2023 katika gulio la Kijiji cha Ikindilo mshtakiwa alimtorosha binti chini ya miaka 16 na kuishi nae kama mume na mke kwa muda wa siku 25.

Aidha mnamo tarehe 07/07/2023 mshtakiwa huyo alimpigia simu mzazi wa binti huyo  kwa lengo la kumfahamisha na lengo la kumuoa binti huyo ambae ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza,ambapo mzazi huyo alitoa taarifa jeshi la Polisi na kufanikisha kukamatwa mtuhumiwa mnamo tarehe 08/07/2023.

Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliita  mashahidi wawili upande wake baada ya mashahidi sita na vielelezo vitatu kutoka upande wa mashtaka kukamilika, ndipo mahakama ilipobaini mshtakiwa anamakosa na kumtia hatiani.

 Upande wa mashtaka uliomba mahakama hiyo itowe  adhabu kali kwa mtuhumiwa huku mtuhumiwa akiomba apunguziwe adhabu kwani ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo na wala hakukusudia sema tu Shetani alimpitia akajikuta amefanya hivyo.

Akitoa hukumu hiyo mbele ya mahakama ya Wilaya hakimu mkazi mwandamizi Mhe. Roberth Petro Kaanwa  mara baada ya kusikiliza pande zote za Mashtaka na Mtuhumiwa bila kuacha shaka yoyote ndipo sasa akamhukumu mshtakiwa Malimi Masunga  kwenda Jela  kwa makosa matatu ambayo ni kumtorosha binti chini ya miaka 16 ambapo ni kinyume na kifungu cha 134 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022,Kosa la pili Ubakaji ambapo ni kinyume na kifungu cha 130(1)(2)e na 131(1) vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na kosa la tatu ni Kushawishi kuoa mwanafunzi ambapo ni kinyume na kifungu cha 60A(4) cha sheria ya elimu sura 353 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2016 ambapo kwa ujumla atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.