Sibuka FM

DC Maswa atangaza kiama kwa wakandarasi wazembe

10 April 2024, 6:00 pm

Pichani ni Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge mwenye shati la mikono mirefu akikagua Moja ya daraja Ambalo lipo kwenye matengenezo Picha na Samwel Mwanga

Hatuwezi kuwa na wakandarasi wazembe namna hii ambao hawafanyi kazi kwa mujibu wa mkataba na hawajui ni adha gani ambayo wananchi wanaipata  nishauri serikali imfute mkandarasi na kampuni yake hiyo katika orodha ya Wakandarasi hapa nchini.

Na ,Daniel Manyanga

Mkuu wa Wilaya ya Maswa  mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge amemfukuza kazi  Mkandarasi wa Kampuni ya ASA GENERAL SUPPLIERS AND CONSTACTION Co Ltd ya  Bunda mkoani Mara katika wilaya hiyo kutofanya kazi kutokana na kushindwa kutekeleza kwa wakati matengenezo ya barabara na ujenzi wa daraja ambao alikuwa anatekeleza wilayni hapo.

Kaminyoge amechukua uamuzi huo mnamo Aprili 9 mwaka huu alipotembelea mradi huo kwa lengo la kukagua matengenezo ya barabara ya Njiapanda ya Muhida na Jihu iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 57,127,650/=  akiambatana na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo.

Kaminyoge ameongeza kuwa mkandarasi huyo amepewa tenda za Ujenzi wa daraja la Wigelekelo katika barabara ya Mwasayi-Masela-Wigelekelo lenye thamani ya sh 51,707,935 na Matengenezo ya barabara ya Bushashi-Ipililo yenye gharama ya Sh 130,277,000  ambapo mkandarasi ameshindwa kutekeleza kwa wakati kazi zote alizoziomba na kupewa na kusababisha wananchi wa maeneo hayo kupata changamoto kubwa ya usafiri.

Aswege Kaminyoge akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ipililo amesema kuwa hawezi kumvumilia mkandarasi huyo kutokana na kushindwa kufanya kazi hizo licha ya kuitwa mara kwa mara na uongozi wa wilaya na kupewa maelekezo lakini amekuwa hatekelezi licha ya serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu imetoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya miundo mbinu hiyo ya barabara.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Maswa , Aswege Kaminyonge akitoa maelezo ya kumfuta kazi mkandarasi huyo

Aidha mkuu huyo wa wilaya amemwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA)wilaya ya Maswa kufanya manunuzi ya haraka ndani ya wiki moja kuhakikisha barabara ya Bushashi-Ipililo inapitika na maeneo korofi katika barabara ya Njiapanda-Muhida-Jihu yanafanyiwa marekebisho ndani ya kipindi cha siku tatu ili kuondokana na adha wanayoipata wananchi katika maeneo hayo.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Maswa , Aswege Kaminyonge akimtaka meneja TARURA wilaya

Kwa upande wake Meneja wa Tarura wilaya ya Maswa, Mhandisi Justine  Lukanga amesema kuwa Mkandarasi huyo amekuwa anafanya kazi bila kuangalia mkataba wake unasemaje hivyo kushindwa kumaliza kwa wakati miradi ambayo anatekeleza huku TARURA walikuwa wakiandaa taratibu za kumfukuza kwani wamemwita mara kwa mara kuhudhuria vikao vyao(Site Meeting)zaidi ya mara tatu lakini hakuweza kuhudhuria .

 Mhandisi Lukanga amesema kuwa kelele zimekuwa ni kubwa katika wilaya hiyo hasa za ubovu wa barabara kutokana na Mkandarasi huyo kushikilia sehemu kubwa ya kazi hizo na hivyo kushindwa kuzitekeleza hivyo anapaswa kufukuzwa.

Sauti ya meneja TARURA wilaya ya Maswa , Mhandisi Justine Lukanga