Sibuka FM

Maswa: Zaidi ya wananchi Mia Tatu wamepata chanjo ya covid-19 wilayani Maswa mkoani Simiyu

22 June 2023, 2:15 pm

Kwenye picha  ni mkuu wa kitengo cha Usafi,Afya na Mazingira wilaya ya Maswa ,Budodi Walwa akimpatia chanjo ya Covid-19 mmoja wa wananchi wilayani hapo

Na Alex.F.Sayi.

Zaidi ya Wananchi Mia Tatu Wilayani Maswa Mkoani Simiyu  wamepata chanjo ya Covid-19 kufuatia mpango wa halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa afya kuanzia mwezi January hadi April mwaka huu.

Hayo yamesemwa na  mratibu wa chanjo  Wilaya ya Maswa, Abel Machibya ,ambapo amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wamechanja kwa 102% nakuvuka lengo walilopangiwa na Serikali hali iliyosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya  maambukizi ya Ugonjwa huo Wilayani hapa.

Machibya ameongeza kuwa idadi hiyo ya wananchi kupatiwa chanjo ya Covid-19 iliongezeka kufuatia uwepo wa vipindi vya elimu ya chanjo kupitia Sibuka Fm kwa ufadhili wa Internews na TADIO hali ambayo imewezesha kufikiwa kwa wananchi kwa urahisi na kuweza kuchanja zaidi ya wananchi Mia Tatu wilayani hapa.

“Uwepo wa wadau wa Afya Internews na Tadio wamechanjia sehemu kubwa sana katika kufikisha elimu hii kwa wananchi wetu ambao wengi wao walikuwa wakisita kupata chanjo hii kutokana na kutokuwa na imani na chanjo hii’’.Amesema Machibya.

“Kuanzia mwezi wa January hadi April halmashauri ya wilaya ya Maswa tulikuwa na wananchi 350 walipata chanjo ambapo halmashauri kwa kushirikiana na Sibuka fm kwa ufadhili wa wadau wa afya kama Internews na TADIO kupitia vipindi vya afya tumefanikiwa kuongeza idadi ya wananchi kupata chanjo hii  ,lakini bado halmashauri tunaandaa kampeni nyingine na hii itawafikia wananchi wengi Zaidi hivyo tunawaomba wadau hawa wa afya watushike mkono kwenye kampeni hii ya kuwapatia chanjo ya Covid-19 kwa wananchi’’.Amesema Machibya

Modesta Ndamo ,ni Mkazi wa Mjini Maswa mwenye Umri wa miaka (76)  akizungumzia uzoefu  alioupata kwa  mwaka mmoja sasa toka apate chanjo ya Covid-19 amesema kuwa  hali ya Afya yake kwa sasa  inaendelea vizuri na hajapata shida yoyote ile  kiafya tangu achanje Chanjo hiyo ya Covid 19 mwaka mmoja uliopita.

“Kumekuwepo na taarifa nyingi sana huku kwenye jamii yetu ambazo hazina ukweli wowote juu ya chanjo ya Covid-19 wengi wakidai ni mpango wa Wazungu kuimaliza Afrika,mimi nilipopata chanjo hii nililazimika kujificha nikiogopa kuchekwa na jamii lakini elimu ya mara kwa mara imenisaidia sana kujiamini ’’ .Amesema Ndamo

“Mwanzoni kabisa Corona inaingia hapa nchini hakukuwa na elimu ya kutosha kwa wananchi lakini tuwashukuru sana wadau wa afya kupitia Sibuka fm imenifanya nipate chanjo baada ya kuwa na uelewa zaidi juu ya chanjo hii toka nimepata ya chanjo ya Covid-19 hivi sasa ni miezi 6 lakini sijaona mabadiliko yoyote yale ya kiafya’’. Amesema Issa Mathias