Sibuka FM

Simiyu:serikali ya mkoa wa Simiyu kufufua viwanda viwili vya pamba

21 February 2022, 3:47 pm

Kwenye picha ni mkuu wa mkoa wa Simiyu ,David Kafulila aliyesimama kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge aliyekaa mwenye suti nyeusi kulia ni mwenyekiti wa bodi ya ushirika mkoa wa Simiyu (SIMCU) huku waliopo nyuma ni kamati ya ulinzi na usalama mkoa.

Na mwandishi,Daniel Manyanga,Simiyu

Serikali mkoani Simiyu inatarajia kufufua viwanda viwili ambavyo vilijengwa wakati wa ukoloni lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi hususani wakulima wa zao la pamba kupata huduma na soko la karibu.

Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Simiyu David kafulila wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali wilayani Maswa mkoani hapo na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya rais Mhe.Samia Suluhu Hassan imedhamilia kuwakomboa wakulima wa pamba nchini.

Kafulila amesema kuwa wanaenda kufufua viwanda viwili kiwanda kimoja ni kwa ajili ya kukamua mafuta ya pamba cha “Lugulu ginnery” kilichopo wilayani Itilima na cha pili ni “Sola ginnery” kilichopo wilayani Maswa ambacho hiki kitakuwa cha kuchambua pamba na tayari serikali ya awamu ya sita imeshatoa maelekezo ya kufufuliwa kwa viwanda hivyo.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Simiyu ,Davida Kafulila akizungumza na baadhi ya wajumbe aliambatana nao kwenye ukaguzi wa kiwanda cha kuchambua pamba cha Sola ginnery

Kafulila ameongeza kuwa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya rais Mhe.Samia Suluhu Hassan haitaki ujanja ujanja kwenye pamba na itaendelea kushughulika na wale wote wanaohujumu ushirika hapa nchini.

Awali akisoma taarifa kwa niaba ya meneja wa chama kikuu cha ushirika(SIMCU)  wilaya ya Maswa afisa ushirika wilayani hapo Cosmas Budodi amesema kuwa kiwanda hicho “Sola ginnery” cha kuchambua pamba kilijengwa na waasia na kikaanza kufanya kazi kipindi cha ukoloni mnamo mwaka 1958 na badae kununuliwa kutoka kwa waasia kwenda kwa Victoria federation kisha kukabidhiwa rasmi mnamo mwaka 1959 na badae kukabidhiwa katika chama kikuu cha ushirika mkoa wa Simiyu(SIMCU) mnamo mwaka 2021 kufuatia kuanzishwa kwa mkoa wa Simiyu.

Aidha Budodi ameiomba serikali kusaidia utatuzi wa baadhi ya changamoto zinazokikabili kiwanda hicho ili kusaidia uendeshaji wa shughuli pindi kitakapoanza kufanya kazi katika msimu huu wa pamba.

Katika hatua nyingine Davida Kafulila amelidhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tanki la kusambazia maji wilayani hapo  lenye ujazo wa lita milioni moja ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 80.