Sibuka FM

Maswa:Mwanri atolea ufafanuzi kuporomoka kwa bei ya zao la Pamba Nchini.

11 July 2023, 8:08 pm

Pichani ni Mkurungenzi wa Halmashauri ya Wilaya Maswa Maisha Mtipa akiwa ameshikilia Dhababu nyeupe (Grade one) karibu yake ni Diwani wa kata ya Mwamashimba Daud S.Dila. Picha na Alex Sayi.

Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imeweza kuvuka lengo la  uzalishaji wa zao la  Pamba kwa msimu wa mwaka 2022/2023 kwa kuzalisha  kwa zaidi ya 106.35% ya uzalishaji uliotarajiwa.

Na,Alex Sayi.

Balozi wa zao la Pamba Nchini Agrey Mwanri amebainisha sababu zilizopelekea kushuka kwa bei kwenye zao hilo la Pamba Duniani kwa msimu wa kilimo 2022/2023.

Mwanri amesema kuwa kushuka kwa bei ya zao hilo imetokana na Nchi nyingi Dunia kuanza kuzalisha zao hilo baada ya kupungua kwa tishio la janga la Covid-19  hivyo kuathiri mwenendo wa bei wa zao hilo kwenye soko la dunia.

 Mwanri amebainisha hayo wakati akizungumza na wakulima katika kijiji cha Dodoma kata ya Mwamashimba Wilayani Maswa Mkoani Simiyu akiwa ziarani Mkoani hapa ziara iliyolenga kuwaelimisha wakulima hao namna ya uvunaji wa  Pamba yenye ubora  itakayoweza kushindanishwa kwenye soko la Dunia.

Sauti ya Agrey Mwanri
Balozi wa zao la Pamba Nchini Agrey Mwanri akitoa ufafanuzi kwa Wakulima wa Kijiji cha Dodoma Kata ya Mwamashimba sababu zilizopelekea kushuka kwa bei ya zao hilo Nchini.Picha na Alex Sayi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Aswege Kaminyoge amewataka maafisa kilimo,watendaji ngazi ya Wilaya na Vijiji kuhakikisha wanasimamia sheria za ulimaji wa zao hilo na kutoa elimu kwa wakulima ili wakulima hao waweze kulima kilimo chenye manufaa tofauti na ilivyo kwa hivi sasa.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge

Maisha Mtipa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa amewataka wakulima hao kuzingatia maelekezo waliyopewa na Balozi wa zao hilo ili waweze kunufaika na kilimo hicho na kuongeza kuwa Halmashauri hiyo itahakikisha inasimamia maelekezo yaliyotolewa ili kilimo hicho kiwe na tija kwa mkulima

Sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Maisha Mtipa.

Afisa Mazao Wilaya ya Maswa Mabula Yohana amesema kuwa Halmashauri  hiyo imeshavuka lengo lililokuwa limekusudiwa kwenye uzalishaji wa zao hilo la kimkakati kwa  kulima ekari 87,438.06 sawa na 106.35% kati ya ekari 82,212.4 zilizokusudiwa kwa mwaka wa kilimo 2022/2023.

Sauti ya Afisa Mazao Wilaya ya Maswa Mabula Yohana

Akizungumza na Sibuka fm, Salu Mashomari mkulima na mkazi wa kijiji cha Dodoma amesema kuwa bei elekezi ya Sh.1060 imewakatisha tamaa wakulima hao kulingana na matarajio waliyokuwa nayo kuwa huenda msimu huu bei ya Pamba ingekuwa mara mbili ikilinganishwa na msimu wa mwaka jana.