DC Maswa Atoa Siku 14 Watendaji Kukabidhiana Ofisi
4 April 2024, 3:02 pm
Watendaji wote waliotajwa kula fedha za maendeleo zitokanazo na michango ya Wananchi ndani ya siku kumi na Nne warudishwe Ili kuja kujibu tuhuma na kufanya makabidhiano Mbele ya Serikali ya Kijiji.
Na, Daniel Manyanga
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Aswege Kaminyoge ametoa siku kumi na nne kwa Watendaji katika Kijiji na kata ya Bugalama waliowahi kufanya kazi hapo kurudishwa mara moja ili kuja kujibu tuhuma zinazowakabili za utafunaji wa fedha za maendeleo zilizochangwa na Wananchi pamoja na kufanya makabidhiano mbele ya Serikali ya Kijiji.
Kaminyoge ametoa agizo hilo kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa Wakati wa Mkutano ya Hadhara wa kusikiliza kero mbalimbali za Wananchi na kuweza kuzitafutia utatuzi ili kuweza kuondoa kero kwa jamii na kuendelea kusimamia dhana ya Utawala Bora
Aswege Kaminyoge amesema kuwa Watendaji wanaotajwa na Wananchi kutafuna fedha za maendeleo zinazotokana na michango ya Wananchi kijijini hapo lazima warudishwe mara moja ili kuja kujibu tuhuma hizo pamoja na kufanya makabidhiano mbele ya serikali ya kijiji hicho ili wananchi wapate nafasi ya kuhoji michango yao imefanya kazi gani huku Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Utumishi nao wakitakiwa kuwepo kwenye makabidhiano pamoja na mkutano huo.
Awali Robert Machiya mkazi wa kijiji cha Bugalama alipata nafasi ya kuwasilisha kero yake kwa mkuu wa wilaya hiyo ambapo alihoji ni sheria ipi inayompa mamlaka Mtendaji wa Kijiji au kata kutafuna fedha za maendeleo zinazotokana na michango ya Wananchi katika kijiji au Kata moja na kuhamishiwa kijiji/kata nyingine tena hata bila ya kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.