Sibuka FM
Sibuka FM
5 May 2025, 17:24

“Tusikilize hoja za wakulima wa pamba na tuzifanyie kazi maana kuna siku uzalishaji wa zao hilo utakuja kushuka na mwisho tutaanza kumtafuta mchawi ni nani wakati sisi ndiyo tulikuwa watu wa kwanza kufifisha juhudi za wakulima wetu kwa kitu kidogo tu cha bei ya zao hilo ni kweli kuna uwezekano bei ya soko la dunia ipo chini lakini wizara ya kilimo mwaweza kufanya jambo ili walau kuleta uhalisia wa nguvu wanazotumia wakulima wetu.”
Na, Daniel Manyanga
Siku chache baada ya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia wizara ya kilimo kutangaza bei ya pamba katika msimu wa ununuzi wa mwaka 2025/26 wilayani Bariadi wakulima wa zao hilo wameomba kuongezewa kwa bei ili iweze kuleta uhalisia wa gharama wanazotumia wakati wa kilimo.
Wakizungumza na Sibuka Fm kwa nyakati tofauti baadhi ya wakulima hao wamesema kuwa bei iliyotangazwa mnamo Mei mbili mwaka huu katika kijiji cha Mwakibuga na mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi haina faida kwa mkulima huyo ukilinganisha na gharama wanazotumia wakati wa kilimo hadi kufikia mavuno yake.

Wakulima hao wameomba serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kuangalia tena upya swala ya bei iliyotangazwa ya shilingi 1150 kwa pamba daraja la kwanza huku daraja la pili ni shilingi 575 iweze kuongezeka walau ifike shilingi elfu mbili kwa kilo ili kuweza kuleta uhalisia ukilinganisha na gharama zinazotumika katika kilimo cha zao hilo.
Awali akizungumzia na wakulima wa zao la pamba wakati wa ufunguzi wa msimu wa manunuzi mkuu wa wilaya ya Baraidi, Simon Simalenga amewataka wakulima kuuza pamba iliyo safi na bora ili wao kama viongozi wao wakienda kuwatetea bei kupanda wawe na hoja za msingi kwa bei kupanda ili wakulima hao waweze kujichamua kiuchumi kutokana na kilimo cha zao hilo.