Sibuka FM
Sibuka FM
20 May 2026, 00:23

Kwasasa wilaya ya Meatu tumepiga marufuku uvunaji wa pamba kwa kutumia vikundi vya ngoma na muziki maana havizingatii kanuni bora za pamba hali inayosababisha uchafuzi wa pamba wakati wa uvunaji ” Thomas Shilabu afisa kilimo wilaya ya Meatu.
Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS ), maafisa kilimo wa program ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) pamoja na makampuni ya ununuzi wa zao la pamba wilayani Meatu mkoani Simiyu wamepewa mafunzo ya namna ya kusimamia usafi na ubora katika zao la pamba ili kuleta tija katika soko la kimataifa
Hayo yameelezwa na mkuu wa divisheni ya kilimo na mifugo wilayani hapo ndugu Thomas Masanja Shilabu kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Meatu Mhe Fauzia Hamidu Ngatumbura na kusema kuwa wakulima wamekuwa wakiharibu ubora kwa kutokuzingatia kanuni nzuri za uvunaji na badala yake kutumia ngoma na muziki maarufu kwa jina la kumba kumba hali inayosababisha kuharibu pamba.
Mkuu huyo wa divisheni ya kilimo na mifugo amesema kuwa sheria za pamba zipo hivyo, na kutaka viongozi wa vyama vya AMCOS na BBT wazisimamie ili pamba itakayonunuliwa iwe safi na bora huku akieleza matarajio ya kilo zitakazovunwa katika msimu wa 2026/2027 ni makubwa ukilinganisha na msimu uliopita wa 2025/2026

Penina Range na Sharifa Salum ni wataalamu wa maabara katika kitengo cha usafi na ubora wa pamba kutoka Bodi ya Pamba Tanzania -TCB ambao wamesema kuwa lengo la kutoa semina hizo ni kuhakikisha usimamizi wa usafi na ubora wa pamba unaimarishwa kupitia kwa viongozi wa AMCOS, BBT na wasimamizi wa ununuzi hasa katika msimu huu wa soko.
Aidha wa upande wake mkaguzi wa pamba wilaya ya Meatu Hemed Kabeya amesema kuwa hawatawavumilia viongozi wote watakaofanya ubadhilifu kwa wakulima kwani watawaondoa mara moja huku akiwataka kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuepuka kuingia kwenye migogoro hiyo.
Nao viongozi wa AMCOS na maafisa kilimo wa BBT wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi yale yote waliyoelekezwa kwenye semina ili pamba itakayonunuliwa iwe safi na bora na ifae katika ushindani wa soko la Dunia hivyo hawatakubali kununua pamba chafu.


