Sibuka FM
Sibuka FM
5 June 2026, 22:19

Kila mmoja akitimiza wajibu wake katika kufanya kazi hautakuwa na migogoro yoyote, Lakini kwasababu tunafanya kazi kwa matakwa ya watu fulani ndio maana inafikia hatua ya mizozo kama hii ” Bi Caroline Shayo -Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo Maswa “
Wenyeviti wa vitongoji vinavyounda mamlaka ya mji mdogo Maswa, Mkoani Simiyu wamelalamikia ubovu wa barabara kutopitika hasa kipindi hiki baada ya mvua za masika kuziharibu licha ya kuwa vitongoji hivyo kuwa Maswa mjini hali inayopelekea ucheleweshwaji wa maendeleo.
Hayo yamesemwa na wajumbe hao katika kikao cha baraza la mamlaka ya mji mgodo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika Ukumbu wa ofisi za mamlaka zilizopo mtaa wa Ujenzi maswa mjini
Wajumbe hao wamesema kuwa Wakala wa barabara za Vijijini – TARURA wamekuwa hawashirikishi viongozi wa vijiji na vitongoji wakati wa kubaini vipaumbele vya barabara katika maeneo hali inayopelekea kurudia barabara zile zile ambapo zinapitika muda wote

Hali hiyo ilisisitizwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji huo Mhe, Caroline Shayo na kusema kuwa wamekuwa wakiacha kutengeneza barabara zenye vipaumbele na ambazo hazipitiki kabisa hivyo kabla ya kuanza matengenezo washauriane na Diwani husika au viongozi wa vitongoji husika
Akijibu hoja za wajumbe hao, Kaimu meneja wa Tarura Wilaya ya Maswa Mhandisi Baraka Libungo amesema kuwa tayari tarura imetenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara korofi ili zipitike na kuchochea uchumi wa Wananchi wa Maswa
Aidha mwenyekiti wa Mamlaka hiyo Bi shayo akazungumzia suala ya mzabuni wa kukusanya taka katika mji wa Maswa kuwa mzabuni huyo hafai na ameshindwa kukidhi vigezo na matakwa ya kukusanya taka kama walivyotarajia hivyo mamlaka haitaendelea kufanya kazi nae.


