Sibuka FM

Meatu:Operesheni ya vyoo yawakimbiza wananchi uboreshaji wa daftari la kudumu

9 September 2024, 17:48

Pichani ni mmoja wa wananchi akipata maelekezo kutoka kwa afisa mwandikishaji mara baada ya kufika kwa ajili ya kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm.

Uboreshaji wa taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura ndiyo dira halisi na mwanzo wa kupata viongozi bora wanaochaguliwa na wananchi kwa maendeleo ya Taifa letu hivyo hatuwezi kuvumilia vitendo vya kuvuruga zoezi hilo”.

Na, Daniel Manyanga

Ikiwa leo imesalia siku moja pekee kabla ya kuhitimishwa kwa zoezi la uboreshaji wa taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Simiyu, wananchi katika jimbo la Kisesa wilayani Meatu mkoani humo wameshindwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kutokana na kamata kamata katika operesheni inayofanywa katika jimbo hilo kwa watu wasiozingatia sheria za usafi wa mazingira ikiwemo matumizi sahihi ya vyoo.

Wakizungumza mbele ya mbunge wa jimbo hilo, Luhaga Mpina katika ziara aliyoifanya kwa ajili ya kutembelea vituo vya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika kata za Nzanza, Mwabusalu na Tindabuligi, wananchi hao wameeleza namna ambavyo wamekwamishwa kushiriki katika zoezi hilo baada ya kuyakimbia makazi yao wakihofia kukamatwa.

Pichani ni mbunge wa jimbo la Kisesa,Mhe Luhaga Mpina akizungumza kutokana na kuwepo kwa taharuki hiyo jimboni hapo kwa baadhi ya wananchi kushindwa kushiriki zoezi hilo Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm
Sauti ya baadhi ya wananchi wakieleza namna ambavyo wamekosa uhuru wa kushiriki zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura

Baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao mbunge wa jimbo la Kisesa Luhaga Mpina, akatoa siku saba wananchi hao warejeshewe pesa zao walizotozwa faini kama faini ya kutokutii matumizi sahihi ya vyoo na usafi wa mazingira.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Kisesa ,Mhe Luhaga Mpina akitoa siku saba kurejeshewa fedha wananchi waliotozwa kama faini

Aidha Mpina ameeleza hatua atakazozichukua ili kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kuwa na sifa za kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Kisesa, Mhe Luhaga Mpina akielezea hatua atakazo chukuwa ili wananchi wapate na nafasi ya kuboresha taarifa zao.

Akizungumza na Sibuka Fm kwa njia ya simu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu ,Athman Masasi ametoa ufafanuzi juu ya operesheni hiyo ambayo ameeleza kuwa haikulenga kumuonea mtu yeyote hivyo haiingiliani na zoezi la uboreshaji wa taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Sauti ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu akizungumzia oparesheni hiyo ya kukamatwa kwa wananchi.