Sibuka FM

Simiyu kukabiliana na biashara haramu ya binadamu

15 July 2026, 06:32

“Hakuna mtu aliye juu ya sheria ambaye anafikiria atasalimika na mkono wa serikali kutokana na biashara haramu ambazo anafanya tutahakikisha tunathibiti kwa nguvu zote ili kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu”.

Na, Anita Balingilaki

Katika kuhakikisha kuna kuwepo uthibiti wa usafirishaji haramu wa binadamu na uwepo wa uhamiaji salama tayari ndani ya mkoa wa Simiyu kumeundwa kikosi kazi kikihusisha wajumbe mbalimbali wakiwemo kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha elimu inafika kwenye jamii na wahusika wa matukio hayo wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Kikosi hicho kimeundwa baada ya kumalizika kwa semina iliyohusu usafirishaji haramu wa binadamu na uhamiaji salama ikiwa na lengo la kuimarisha juhudi za pamoja katika kuzuia na kupambana na usafirishaji huo na imeandaliwa kupitia mradi wa emPoWeReD II unaotekelezwa na shirika la CVM and APA kwa ushirikiano wa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi,Mahoteli,Majumbani,huduma za jamii na Ushauri (CHODAWU) pamoja na shirika la Wote sawa kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la Italian Agency for Development Cooperation.

Akiongea na wajumbe wa kikosi kazi hicho kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu ACP Edith Swebe amesema changamoto ya usafirishaji haramu wa binadamu si ya taasisi moja hivyo kila mtu kwa nafasi yake anatakiwa kuwa sehemu ya kupinga jambo hilo ili kuwa na sauti ya pamoja katika kupambana nalo.

ACP Swebe amesema waathirika wakubwa wa usafirishaji haramu wa binadamu ni wanawake,watoto na wasichana kupitia ajira kwani wengi wao uishia katika mazingira ya unyonyaji,kazi za kulazimishwa,ukatili na kunyimwa haki zao za msingi huku akisisitiza katika mkoa wa Simiyu changamoto hiyo imeonekana kwenye usafirishaji na ajira za watoto katika sekta zisizo rasmi.

“Ndugu washiriki katika kipindi chote cha semina hii mmejifunza kwa kubadilishana uzoefu mmejadili changamoto zilizopo, mmetafakari suluhisho kwa pamoja lakini kupitia mijadala mbalimbali mmeelewa kwa kina usafirishaji haramu wa binadamu”ACP Swebe.

Mmoja wa wawezeshaji wa semina kutoka wizara ya mambo ya ndani Patricia Temu akiongea na washiriki Picha na Anita Balingilaki
Kushoto ni mkuu wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Simiyu inspector Dionice Katemana na kulia ni mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Bariadi SP Enock Seme wakifatilia kile kinachowasilishwa na mwezeshaji Picha na Anita Balingilaki

Akiongea kwa niaba ya katibu tawala wa mkoa wa Simiyu mganga mkuu wa mkoa huu Dkt Yudas Ndungile amesema moja ya changamoto inayosumbua zaidi mkoani Simiyu ni usafirishaji wa watoto na wasichana kutoka maeneo ya vijijini kwenda kwenye maeneo ya mjini kwaajili ya kupatiwa ajira na mara nyingi ushawishiwa na madalali pamoja na mawakala kwa ahadi za uongo.

Wawezeshaji wa semina na washiriki wakiw kwenye picha ya pamoja na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Simiyu ACP Edith Swebe Picha na Anita Balingilaki

Mwajuma Ally ni mwezeshaji wa semina hiyo kutoka shirika la CVM amesema shirika hilo lilinafanya kazi moja kwa moja na wasichana wanaofanya kazi za majumbani na kundi hilo limekuwa likikutana na usafirishaji haramu wa binadamu lakini kutokana na kuwa na uelewa mdogo wamekuwa hawaelewi hivyo ujio wa mradi wa emPoWeReD II utasaidia kwenye ufumbuzi wa changamoto hiyo kwa kutoa elimu na kuibua matukio na wanaoyatekeleza.

Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Simiyu ACP Chacha Maro akichangia kwenye semina hiyo Picha na Anita Balingilaki
Mkuu wa upelelezi na udhibiti wa mipaka mkoa wa,Simiyu Mrakibu msaidizi wa uhamiaji Aristides Macha akitoa mada kwenye semina hiyo Picha na Anita Balingilaki