Sibuka FM

Mzee Jilala miaka 64 jela maisha kwa kubaka mtoto wa miaka 9 Maswa

13 November 2026, 05:43

Pichani ni Jilala Busanda mzee wa miaka 64 mkazi wa kijiji cha Dulung’wa wilayani Maswa akiwa tayari kwenda kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka mtoto wa miaka 9 Picha na Samwel Mwanga

“Hakuna aliye juu ya sheria ambaye anaweza kufanya vitendo vya hovyo halafu asichukuliwe hatua kali za kisheria lazima kila mtu aishi kwa kutambua kuwa sheria zipo na zinafanya kazi kila siku”.

Na,Daniel Manyanga 

Mahakama ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu ,Jilala Busanda kwenda jela maisha kwa makosa ya mawili ya kubaka mtoto mwenye miaka 9 hukumu iliyotolewa mnamo tarehe 12.11.2026 katika kesi ya jinai shauri na 15102/2026.

Mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa,Mhe.Nhandala Kondela mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi wa polisi,Vedastus Wajanga amemtaja mshtakiwa kuwa,Jilala Busanda, Msukuma mwenye miaka 64 Mkulima mkazi wa kijiji cha Dulung’wa wilayani hapo.

Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi wa polisi, Vedastus Wajanga amesema kuwa mshatakiwa alishtakiwa kwa makosa mawili yote yakiwa ni  kubaka mtoto wa miaka 9 ambapo ni  kinyume na vifungu vya 130(1)(2) (e) na 131(3)  vya sheria ya kanuni ya adhabu  sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

Awali mahakamani hapo ilidaiwa na upande Jamhuri ambao uliwakilishwa na mwendesha mashtaka wa serikali ,mkaguzi wa polisi,Vedastus Wajanga amesema kuwa mnamo tarehe  tofauti mwezi January mwaka 2026 na tarehe 13 mwezi  February 2026 katika kijiji cha Dulung’wa  mshtakiwa alimbaka mtoto mwenye miaka 9 jina lake limehifadhiwa.

Vedastus Wajanga ameendelea kuiambia mahakama kuwa mnamo tarehe 17/06/2026 mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa  kituo cha polisi wilaya ya Maswa na alipohojiwa alikana kutenda  kosa hilo baada ya upelelezi kukamilika mshatakiwa alifikishwa mahakamani na kusomewa makosa mawili ya kubaka  ambapo aliendelea kukana kufanya kosa hilo.

Upande wa jamhuri ulileta jumla ya mashahidi  wanne walitoa ushahidi wao ukiwemo ushahidi wa muhanga ambaye alithibisha kubakwa zaidi ya mara moja na mshtakiwa pindi walezi wake walipokuwa shambani kwa shughuli za kilimo pamoja  vielelezo vinne (04) vilitolewa ikiwepo PF3 ya muhanga

Kwa upande mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea mahakamani hapo alikana kutenda kosa hilo na kudai kuwa hizo ni chuki tu zinazotokana na umiliki wa maeneo na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni mzee wa miaka 64 na ni kosa lake la kwanza huku upande wa mashtaka wakiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye nia mbaya ya kufanya vitendo hivyo vya kinyama ambavyo vinaacha kovu kubwa kwa muhanga

Akitoa hukumu hiyo baada ya kujiridhisha bila kuacha shaka yoyote kutoka pande zote mbili za jamhuri na mshtakiwa hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa, Mhe.Nhandala Kondela akamhukumu, Jilala Busanda kwenda jela maisha kwa makosa mawili ya kubaka pamoja na kulipa fidia muhanga kiasi cha Tsh.700,000/= huku adhabu zote hizo atazitumikia kwa pamoja.