Sibuka FM
Sibuka FM
5 November 2026, 05:26

“Ni kweli elimu ni urithi pekee ambao mwanadamu hawezi kuibiwa wala kusingiziwa hivyo tunakila sababu ya kuwekeza kwenye elimu kuanzia miundombinu na hii itakuwa chachu ya kufikia malengo”.
Na Daniel Manyanga
Katika kukabiliana na upungufu wa miundombinu mashuleni benki ya CRDB imekabidhi madawati 80 katika Shule ya msingi Goriku B na Shule ya Sekondari Ikungulyambeshi zilizopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu ili kusaidia wanafunzi kusoma kwa utulivu pamoja na kurahisisha utendaji kazi kwa Walimu ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Akikabidhi madawati hayo kwa mkuu wa wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga meneja wa benki ya CRDB kanda ya Ziwa,Denis Mwoleka amesema kuwa benki hiyo imekuwa na utamaduni wa kufanya hivyo mara kwa mara siyo tu mashuleni wanafanya hivyo hata taasisi zingine kulingana na uhitaji ili kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili lengo ni kufikia malengo husika.
Wakizungumza na Sibuka Fm, Stephano Marco,James Ngwata na Zabron Mapindo wakazi wa kijiji cha Ikungulyambeshi kata ya Kilalo katika hafla ya kupokea madawati 40 yaliyotolewa na benki ya CRDB shuleni hapo ambapo wamesema kuwa licha ya jitihada wanazoendelea kuzifanya kwa ajili ya kumaliza tatizo la upungufu wa madawati katika shule hiyo bado wanahitaji michango kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kumalizika kwa upungufu wa miundombinu hiyo.
Minza Maduhu ni mkuu wa shule ya sekondari Ikungulyambeshi amesema kuwa pamoja na upungufu wa madawati pia shule hiyo inakabiliwa na changamoto zingine zinazohitaji ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani hao hivyo ameendelea kuwaomba wadau wa elimu kuwezesha miundombinu.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bariadi ,Simon Simalenga akaagiza halmashauri ya wilaya ya Bariadi kuhakikisha inazishughulikia changamoto zilizotajwa kuikabili shule hiyo ili kuleza mazingira rafiki ya utendaji kazi.
