Sibuka FM
Sibuka FM
31 October 2026, 05:36

“Lishe bora ni msingi bora wa afya imara na katika nchi yoyote ile uchumi unajengwa na afya za watu huwezi kustawi halafu watu wako wapo hoi kiafya”.
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Simon Simalenga ameitaka jamii wilayani humo kuzingatia kanuni za lishe bora, na kuhakikisha inawapatia chakula chenye virutubisho akina mama wajawazito , wanaonyonyesha na watoto ili kuwawezesha kuwa na afya bora na kuwasaidia watoto kuepukana na tatizo la udumavu lengo kuwa na kizazi bora chenye afya imara na uchumi thabiti.
Akizungumza na Sibuka Fm katika maadhimisho ya kitaifa ya siku ya lishe kwa halmashauri ya mji wa Bariadi, yaliyofanyika katika mtaa wa Mbiti,Simon Simalenga amezitaja athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kutozingatia lishe bora hivyo kuiomba jamii kuwekeza zaida katika masuala lishe ili kuondokana madhara yanayoweza kutokea kufuatia kukosa lishe bora.
Lilian Festo ni afisa lishe wa halmashauri ya mji wa Bariadi amesema kuwa serikali wilayani hapo inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na elimu sahihi juu ya masuala ya lishe lengo ni kuondoa udumavu katika jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi mjini hapo,Abubakari Sixtus, Mbuke Sungwa, Veronica Sayi, wakaomba maafisa lishe kuendelea kuwatembelea hususan katika maeneo ya vijijini na kuwapatia elimu itakayowasaidia kupata uelewa mzuri wa masuala ya lishe.