Sibuka FM
Sibuka FM
19 August 2026, 22:36

“Ndiyo kila nafsi itaonja mauti lakini kifo cha Samike kimezua simanzi katika kijiji cha Gulumwashi huku wananchi wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi na hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa”.
Na,Daniel Manyanga
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano, Samike Mponeja, mkazi wa Kijiji cha Gulumwashi, Kata ya Malampaka wilayani Maswa, mkoani Simiyu, ameuawa kikatili baada ya kutekwa na watu wanaodaiwa kutaka kulipwa shilingi milioni 7 kutoka kwa wazazi wake ili kumuachia mtoto huyo ambaye ni marehemu kwa sasa.
Mwili wa mtoto huyo umepatikana leo, Agosti 19, 2026, ukiwa umetundikwa juu ya mti katika eneo la kichaka, siku 13 baada ya kutoweka alipokuwa akichunga ng’ombe za nyumbani kwao.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt.Vicent Anney amesema kuwa wahusika wote lazima wawajibishwe kwa mujibu wa sheria zetu za nchi huku wananchi wakitakiwa kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapobaini viashiria vya uhalifu katika jamii ili matukio kama hayo yasijirudie wilayani humo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Simiyu, kamishna msaidizi wa polisi, Chacha Maro amesema kuwa tayari jeshi la polisi limewakamata watu watatu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani kwa hatua kali zaidi za kisheria.
Maro amewaomba wananchi kuwa watulivu na kushirikiana na polisi ili kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo mapema huku akiwaonya dhidi ya kuchukua sheria mkononi kwa kwenda kuwaadhibu wazazi au ndugu wa vijana wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Akizungumza katika eneo ambako mwili huo umepatikana, Veronica Sospeter mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa mtoto huyo alipotea Agosti 6, 2026 majira ya saa 7:00 mchana wakati akichunga ng’ombe akiwa pamoja na watoto wenzake watatu.
Veronica ameongeza kuwa kabla ya kutoweka mtoto huyo alikutwa na mmoja wa watu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo ambaye alimtuma kwenda kuchukua fimbo katika eneo la kichaka lakini hakurejea tena hadi mwili wake ulipopatikana ukiwa umetundikwa juu ya mti.

Naye kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Gulumwashi, Mabala Shimbi amesema baada ya kupokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo wananchi walianza juhudi za kumtafuta katika maeneo mbalimbali, lakini hawakufanikiwa kumpata.
Hata hivyo ,Mabala Shimbi amesema kuwa baadaye mmoja wa watu waliokamatwa akidaiwa kuhusika na tukio hilo alimpigia simu mama wa mtoto huyo na kumtaka kutoa kiasi cha shilingi milioni 7 akidai mtoto wake ametekwa na watekaji wanataka hiyo fedha ili waweze kumuachilia mtoto huyo.

