Sibuka FM
Sibuka FM
15 September 2026, 07:02

“Ukuaji wa uchumi unachangiwa pakubwa sana na uimara wa miundombinu yetu haiwezekani uwe na uchumi imara halafu miundombinu yako ni mobovu tunataka kila sehemu pawe bora ili kwenda kwenye dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050”.
Na,Daniel Manyanga
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Simiyu limetakiwa kuhakikisha linasimamia kikamilifu ujenzi wa kituo cha kupozea umeme unaoendelea katika eneo la Imalilo wilayani Bariadi mkoani humo ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kuwawezesha wakazi wa mkoa wa Simiyu kuwa na umeme wa uhakika.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Simiyu Said Mtanda baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa mradi huo na kukagua maendeleo yake, ambapo amewataka TANESCO mkoani hapa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mradi huo pamoja na ule wa njia ya kusafirisha umeme unakamilika kwa wakati na uanze kuwanufaisha wananchi na kuondokana na adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Mhandisi Twaha Kigangama ni meneja wa TANESCO mkoa wa Simiyu, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utawawezesha wakazi wa mkoa wa Simiyu kupata umeme toshelevu na kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Kwa upande wake mhandisi wa mradi wa kituo cha kupozea umeme ,Daniel Katto, ameeleza kazi zitakazofanyika kupitia mradi huo huku Hellen Ntelemko na Hassan Gumalija wakazi wa mkoa wa Simiyu wakiomba kufikishiwa huduma ya umeme hadi vitongojini pamoja na kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi bila kuwa na wasiwasi wa kukata kwa miundombinu hiyo.