Sibuka FM
Sibuka FM
8 September 2026, 17:50

“Hakuna aliye juu ya sheria za nchi kila mtu yupo chini sheria na katiba ya nchi hivyo biashara haramu lazima zikomeshwe kwa namna yoyote ile katika jamii zetu na wahusika wachukuliwe hatua kali zaidi za kisheria “.
Na ,Anita Balingilaki
Katika kuhakikisha jamii inafikiwa na kutambua viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu mkoa wa Simiyu uliunda kikosi kazi kwaajili ya kukabiliana na changamoto hiyo na mara baada ya kuundwa kikosi hicho kilipitisha kwa kauli moja mpango kazi kwaajili ya utekelezaji wa shughuli hiyo.
Mpango kazi huo utatumika kwa kipindi cha mwaka mmoja na utajumuisha utoaji wa elimu kwenye jamii ambayo itakuwa sehemu ya kukabiliana na usafirishaji huo.
Mwajuma Ally ni mwezeshaji kutoka shirika la Community of Volunteers for the World (CVM) kupitia mradi wa emPoWeReD II ambao unaenda kuwasaidia wafanyakazi wa majumbani kwa kuwajengea uwezo na pia kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu.
Kupitia mradi huo CVM wanashirikiana na wadau wengine na wizara ya mambo ya ndani ya nchi kupitia sekretarieti ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu (ATS).
“Leo mpango kazi umetengenezwa na unaenda kusainiwa uwe rasmi kutumika kwa mkoa wa Simiyu na unaenda kutumika kwenye mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu ili mambo yote yanayoendana na changamoto hiyo yapatiwe ufumbuzi”Mwajuma Ally.
Baada ya mpango kazi huo matarajio ya kikosi kazi hicho ni kupata mafanikio makubwa kwa kuifikia jamii kwa kuipatia elimu kuhusu viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu na madhara ambayo yatampata mhanga wa vitendo.
“Elimu itasambaa kwa watu kupitia kikosi kazi na nimatarajio yetu jamii itaelewa na kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo”Boniface Bahame,afisa kazi kutoka idara ya kazi mkoa wa Simiyu.
“Kutokana na elimu niliyoipata kuhusiana na usafirishaji haramu wa binadamu naamini mimi nitakuwa chachu ya mabadiliko kwa wenzangu na jamii inayonizunguka na hii itakuwa hatua nzuri ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo” Janeth Festo.
