Sibuka FM
Sibuka FM
16 September 2026, 20:10

“Tunatakiwa kujiandaa mapema kwa mamlaka zote katika kukabiliana na athari za El Nino ikiwemo kuandaa miundombinu yetu kama barabara, vitendeakazi ili kama ikitokea basi iwe rahisi kufika katika maeneo yaliyoathirika”.
Na,Daniel Manyanga
Waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka mamlaka zinazohusika na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini kuhakikisha zinaimarisha miundombinu ili kuepuka athari za mvua El Nino ambazo zinatarajiwa kunyesha mwaka huu kutokana na utabiri wa hali ya hewa kutoka mamlaka ya hali ya hewa nchini(TMA).
Waziri mkuu ,Dkt.Mwigulu Nchemba ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya mkoani Simiyu ambapo amesema kuna haja kubwa kwa kila mamlaka zinazohusika na ujenzi wa miundombinu kukagua na kuboresha sehemu zenye changamoto ili kuondokana na adha za El Nino kama ikitokea.
Krypton Mmanga, Nickson Mahenge na Hawa Idd ni baadhi ya wakazi wa mkoa wa Simiyu wameeleza kuwa kutokana na maelekezo yanayoendelea kutolewa na mamlaka ya hali ya hewa pamoja na viongozi mbalimbali nchini ipo haja ya serikali kuweka mifumo na mipango madhubuti itakayosaidia kuepusha athari kwa wananchi pindi mvua hizo zitakapoanza kunyesha.
Naye kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu, mrakibu msaidizi wa jeshi la zimamoto na uokoaji Faustin Mtitu, amewata wakazi wa mkoa wa Simiyu kuendelea kuchukua tahadhari kwa ajili ya kujiepusha na athari za El Nino.