Sibuka FM
Sibuka FM
21 August 2026, 14:26

“Wananchi wasituone kama maadui wao kama wanavyotafsiri watu wengine polisi na raia ni ndugu hakuna utofauti wowote hata polisi ni kazi tu lakini kuna siku atasitaafu kazi na kurudi kwenda kuishi na wananchi wa kawaida”.
Na,Daniel Manyanga
Katika kuadhimisha miaka 20 ya polisi jamii jeshi la polisi wilayani Maswa mkoani Simiyu limefanya matendo ya huruma katika hospitali ya wilaya ya Maswa pamoja usafi wa mazingira ikiwa ni ishara upendo kwa jamii na kuimarisha uhusiano.
Akizungumza na Sibuka Fm wakati wa maadhimisho hayo mkuu wa kituo cha polisi wilaya,mrakibu wa polisi (SP) ,Ramadhani Mkimbu amesema maadhimisho ya miaka 20 ya polisi jamii yamewapa fursa ya kwenda moja kwa moja kwa wananchi na kushiriki shughuli zenye manufaa kwa jamii.
Mkimbu amesema kuwa jeshi la polisi wilayani hapo katika kuadhimisha miaka 20 ya polisi jamii wamefanya matendo ya huruma kwa wahitaji pamoja usafi wa mazingira katika hospitali ya wilaya na kuongeza kuwa askari ni sehemu ya wananchi wanaowahudumia na siyo maadui kama inavyotafsiriwa na baadhi ya watu.
Dkt.Deogratius Mtaki ni mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Maswa amesema kitendo cha jeshi la polisi kufika hospitalini hapo na kushiriki shughuli za kijamii kimeonyesha upendo wa agape kwa wagonjwa waliolazwa na wao kujisikia faraja.
Mtaki ameongeza kuwa hospitali hiyo ina wagonjwa ambao uwezo wao wa kujihudumia ni mdogo hivyo kupitia misaada iliyotolewa na polisi itawasaidia katika kipindi ambacho wanaendelea na matibabu.

Beatrice Julius,Magreth Kadomola ni baadhi ya waliofikiwa misaada hiyo wamelishukuru jeshi la polisi na kuziomba taasisi zingine za kiserikali na binafsi kuiga mfano huo kwa kuwakumbuka watu wenye uhitaji.

Miongoni mwa vitu vilivyotolewa na askari hao ni sabuni za kufulia, mafuta ya kujipaka, pampasi za watoto, dawa za meno, maji na juisi, huku baadhi ya askari wakishiriki pia katika uchangiaji wa damu salama pamoja kufanya usafi wa mazingira eneo la hospitali.

