Sibuka FM
Sibuka FM
27 October 2026, 05:44

“Hatuwezi kuvumilia vitendo vya hovyo viendelee kufanyika kwenye jamii za kuozesha wanafunzi wakiwa na umri mdogo pia wakiendelea masomo yao ,yeyote atakayehusika na vitendo hivyo sheria kali zitachukuliwa dhidi yake ili kukomesha ndoa za utotoni”.
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya Bariadi mkoani Simiyu,Simon Simalenga amemunusuru na ndoa za utotoni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Igaganulwa iliyopo kata ya Dutwa wilayani Bariadi ambaye alitaka kuozeshwa kabla ya kumaliza masomo yake kwa mahari ya ng’ombe 16.
Akizungumza na Sibuka Fm nyumbani kwa mwanaume aliyetaka kumuoa binti huyo ,Simon Simalenga amesema kuwa baada ya kupata taarifa za kikachero walifunga safari na kufika kwa kushtukiza katika hafla iliyoandaliwa kwa ajili ya mwanaume huyo kutoa mahari kwa walezi wa binti huyo na kuongeza kuwa serikali inafanya jitihada kubwa kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu hivyo vitendo vyovyote vya kukwamisha wanafunzi kimasomo havitavumilika wilayani hapo.
Jackson Mangu ni afisa mtendaji wa kata ya Dutwa amesema kuwa vitendo vya kuwakatisha masomo na kuwaozesha mabinti vinatokana na imani potofu ambazo bado zipo katika jamii kutokana na kuamini kuwa kusomesha na mwanamke ni kupoteza muda na kupata hasara kutokana na baadhi ya wanafunzi wa kike kuacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kupata mimba wakiwa shuleni.
Kwa upande wao baadhi ya wafunzi wa shule hiyo,Esther Manyangu, Baraka Luzuga na Calvin Richard wamepongeza juhudi za mkuu wa wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga katika kupigania ndoto za mwanafunzi mwenzao huku wakiomba hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika na mpango huo kuozesha mwanafunzi akiwa masomoni.