Sibuka FM
Sibuka FM
20 November 2026, 05:29

“Hatutarajii kuona kuna kikundi hata kimoja hakijarudisha mikopo ya asilimia kumi kama ikitokea hivyo tutawakamata na kuwafikisha mahakamani ili warudishe hizo fedha na watu wengine waweze kupata na kujikomboa kiuchumi“.
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Simon Simalenga amevitaka vikundi vilivyopatiwa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ya mji wa Bariadi, kuhakikisha vinarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwapatia fursa watu wengine kunufaika na fedha hizo.
Akizungumza na wanufaikaji wa mikopo hiyo ya asilimia kumi itokanayo na mapato ya ndani ya halmashauri katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 mkuu huyo wa wilaya, Simon Simalenga amesema kuwa wale wote watakaoshindwa kurejesha mikopo hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani ili iweze kuwasaidia na watu wengine katika kujiinua kiuchumi kutokana na shughuli wanazozifanya.
Akitoa taarifa ya mikopo hiyo kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Bariadi ,Sylvanus Gwiboha amesema kuwa jumla ya shilingi 104,170,000 zimetolewa na halmashauri hiyo kwa vikundi 12 huku halmashauri hiyo ikitarajia kukusanya zaidi ya billion mbili katika mwaka huo wa fedha na asilimia kumi itaenda kuwanufaisha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Winfrida Masanja, Prisca Msoke na Samuel Charles ni baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo ambao wameeleza namna itakavyowasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi wanazozifanya huku wakiahidi kurejesha kwa wakati ili na watu wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo.