Sibuka FM
Sibuka FM
29 October 2026, 18:06

“Tunahitaji kuona wakulima wa zao la pamba wananufaika na kilimo hicho ili kuweza kuona tija kwa kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka kilo 300 hadi 800 kwa ekari moja.”
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dkt.Vicent Naano Anney amewataka wataalamu wa kilimo kuacha mara moja tabia ya kutegemea posho ili watekeleze majukumu yao hivyo kukosesha mavuno yenye tija kwa wakulima wa pamba wilayani hapo kutokana na kukosekana kwa elimu ya kilimo cha kisasa.
Dkt.Anney ametoa rai hiyo kwa wataalamu wa kilimo wakati wa kikao cha wataalamu wa sekta mbalimbali wilayani hapo kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya zamani na kuongeza kuwa wakiacha kuangalia posho katika utekelezaji wa majukumu itasaidia sana mpango wa kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la pamba kutoka kilo 300 hadi 800 kwa ekari moja.
Maisha Mtipa ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa amesema kuwa katika kutekeleza agenda ya kuongeza uzalishaji wa zao la pamba serikali ya wilaya hiyo imejipanga vyema ili kufikia dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050.

Nao baadhi ya wadau mbalimbali wa kilimo waliohudhuria kikao hicho wakaomba watendaji kuacha kukaa sasa maofisi badala yake watoke ili kuongeza uzalishaji wa pamba na kuweza kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 20250.
