Sibuka FM
Sibuka FM
24 November 2026, 16:36

“Tuendelee kuchukuwa tahadhari kabla ya kuanza kuifanya hiyo kazi lakini pia tupunguzeni tamaa ya fedha maana tunafanya shughuli zingine ambazo hatuna ujuzi nazo mwisho wa siku inabadilika inakuwa maafa”.
Na,Daniel Manyanga
Watu wawili waliofahamika kwa majina ya Shenya Mathias (30) Paschal Shigela (23) wakazi wa mtaa wa Ngh’ami kata ya Nyalikungu wilayani Maswa Mkoani Simiyu wamefariki dunia baada ya kuzama kwenye kisima huku Alfa Zakaria (28) akinusurika kifo walipokuwa wakitoa mbao zilizokuwa zinatumika kwenye ujenzi ndani ya kisima.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu mrakibu msaidizi wa jeshi la zimamoto na uokoaji, Faustin Mtitu amesema kuwa tukio hilo limetokea wakati wanaume hao walipokuwa wanafanya kazi ya kutoa mbao kwenye kisima ambazo zilikuwa zinatumika wakati wa ujenzi.
Katika hatua nyingine jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu limewataka wananchi kuacha mara moja kufanya kazi ambazo hawana ujuzi nazo na kutoa taarifa haraka kwa jeshi hilo kama kuna majanga yanayohitaji uokozi.