Joy FM

Watoto hupotea na kukutwa wamefariki Kasulu

6 June 2024, 10:56

Watoto wakiwa katika mazingira hatarishi. Picha na mtandao

Serikali imetakiwa kufuatilia na kudhibiti vitendo vya watoto kupotea katika mazingira ya kutatanisha katika halmashauri ya mji wa Kasulu hali inayosababisha wananchi kuishi bila amani.

Na Michael Mpunije – Kasulu

Wananchi katika halmashauri ya mji Kasulu mkoani Kigoma wameiomba serikali kuimarisha ulinzi dhidi ya watoto ili kudhibiti suala la baadhi ya watoto kupotea huku wengine wakipatikana wakiwa wamefariki.

Wananchi hao wamesema kuwa kumekuwepo na tabia ya watoto kupotea jambo ambalo linapelekea baadhi ya wazazi kushindwa kuwaagiza sehemu yoyote watoto wao.

Wameshauri pia wazazi kuwa mstari wa mbele kuwaangalia watoto wao kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili vinavyoweza kukatisha ndoto zao.

Sauti ya wananchi waliopotelewa na watoto wao

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amesema watoto ambao wamekuwa wakiripotiwa kupotea baadhi yao wamekuwa wakikutwa wakiwa wamefariki kwa kuzama kwenye visima vya maji na kuwataka wananchi kufunika visima hivyo ili kuepusha madhara zaidi kwa watoto.

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanali Isac Mwakisu. Picha na Michael Mpunije

“Kulikuwa na watoto wengi wanakufa na tunakuta wamekufa lakini uchunguzi wa awali tuligundua kuwa wengi wanaanguka kwenye visima kwahiyo wananchi funikeni visima lakini tunaendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na watu wanaofanya vitendo hivyo vya kuua watoto na kuwapoteza”

Sauti ya Mkuu wa Wilaya Kasulu

Katika hatua nyingine Mkaguzi wa Polisi ambaye pia ni polisi kata wa kata za Mrusi na Nyasha Mubaracka Luwongo alipokuwa akizungumza na wazazi na walezi katika shule ya msingi kasulu amesema atawachukulia hatua za kisheria wazazi watakaobainika kuwatuma watoto wao sokoni majira ya usiku kwamba suala hilo huchangia vitendo vya ukatili kwa watoto.

Sauti ya Mkaguzi wa Polisi kata wilayani Kasulu