Pangani FM
Pangani FM
14 September 2026, 12:06

Afisa Ustawi kata ya Madanga wilayani Pangani Bi Pauline Derik akizungumzia mwamko wa wanaume kuripotii matukio ya ukatili wanayoyapitia . ( picha na Dickson Nghily)
Japokuwa ni nadra kwa wanaume kuripoti kesi za ukatili wa kijinsia, ikiwemo kupigwa na wenza wao, hali hiyo ni tofauti katika Kata ya Madanga, ambapo Afisa Ustawi wa Jamii wa kata hiyo, Bi. Pauline Derick, amesema amekuwa akipokea hadi kesi tano kwa mwezi zinazohusu wanaume wanaoripoti kupigwa na wake zao.
Kwa mujibu wa Bi. Pauline, moja ya sababu zinazopelekea baadhi ya wanaume kupigwa na wake zao ni pale mwanaume anapomweleza mke wake kuhusu nia ya kuoa mke wa pili, jambo ambalo humfanya mwanamke kuwa na hasira.
Bi. Pauline amewataka wanandoa kukaa pamoja na kujadiliana kwa kina kuhusu changamoto zinazowakabili, badala ya kutumia vipigo na vitendo vya ukatili kama njia ya kutatua migogoro.
Amesema vurugu na vipigo ndani ya familia haviathiri wanandoa pekee, bali pia huathiri watoto, ikiwemo kuathiri mwenendo wao wa masomo shuleni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Madanga, Ndg. Makata Mohamed, amesema ingawa kesi za ukatili zipo katika kijiji hicho, suala la wanaume kupigwa na wake zao lilikuwa nadra sana kusikika.
Hata hivyo, amempongeza Afisa Ustawi wa Jamii kwa kazi ya kutoa elimu kwa jamii, akisema hatua hiyo imewasaidia wanaume kuanza kujitokeza na kueleza changamoto wanazokabiliana nazo katika ndoa zao.