Pangani FM

Wazazi wa Pangani na matumizi ya Simu kwa watoto wao.

22 June 2022, 1:31 pm

Wazazi na Walezi Wilayani Pangani Mkoani Tanga wametakiwa kutowapa watoto wao uhuru wa kupitiliza kwenye Matumizi ya simu za mkononi sababu zinaweza kuwa moja sababu ya kuwaharibu kimaadili.

Pangani FM imezungumza na wazazi pamoja na walezi wa kijiji cha Kimang’a kilichopo wilayani humo ambao kwa nyakati tofauti wameeleza uzoefu wao juu ya namna watoto wanaovyoharibika kimaadili kutokana na uhuru ulioptiliza wa matumizi ya simu za mkononi.

Wazazi hao pamoja na walezi wamekemea pia tabia ya wazazi kutokuwa makini katika kufuatilia namna watoto wao wanavyotumia simu za mkononi huku wengine kwa makusudi wakiwapa uhuru watoto wao kutumia simu hizo kama sehemu ya kuonyesha ufahari.

Pia PanganI FM imezungumza na Dk. Vicent Tarimo kutoka Kitengo cha Afya ya Akili katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani ambaye amewataka  wazazi kuwa makini na watoto wao kwa kutowapa uhuru wa kupitiliza kwani matumizi ya simuhizo yana madhara kisaikolojia pia ikiwemo kuwashawishi kufanya vitu vya kikatili kwani bado kwa umri wao hawana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo wanayoyaona.

Naye Bw. Charles Jeremia ambaye ni Mtaalamu wa TEHAMA kutoka Shirika la UZIKWASA amesema ili kumlinda mtoto dhidi ya madhara ya matumizi mabaya ya simu za Mkononi Wazazi wanapaswa kudhibiti wavuti na mitandao ya kijamii katika simu zao hususan ile ambayo hawaruhusiwi kutokana na umri wao kuwa mdogo pamoja na nyingine ambazo ziko kinyume na maadili.

Bw, Charles ameongeza kuwa kwa sasa zipo programu tumizi kwenye simu hizo ambazo zina uwezo wa kudhibiti aina Fulani ya maudhui au mitandao isiyofaa hivyo ni vyema wazazi wakazitumia ili kuwalinda watoto wao.