Pangani FM

Makamu wa Rais kufanya Ziara Wilayani Pangani.

10 March 2021, 7:27 pm

Mkuu wa wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdallah ametangaza ujio wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Wilayani Pangani.

Akizungumza na PANGANI FM leo Bi Zainab amesema kuwa Makamu wa Rais anatarajiwa kuwasili Mkoani Tanga siku ya Jumatatu tarehe 15 Machi 2021 na ataanza ziara katika wilaya za Handeni na Korogwe kisha siku ya Jumanne tarehe 16 ataanzia Wilayani Muheza na kumalizia ziara yake Wilayani Pangani.

Nawahabarisha Wananchi wote wa Pangani kwamba baada ya kusubiri kwa muda mrefu angalau kupata wale viongozi wakubwa kabisa kitaifa naona safari hii mambo yanaenda kutimia, tumtarajie Mama yetu mpendwa na hasa ukizingatia huu ni Mwezi wa Wanawake Duniani kwa hiyo tunampokea Mwanamama wa shoka Makamu wa Rais, ambaye anatarajia kuja Pangani Jumanne tarehe 16 na atakapowasili Wilayani Pangani anatarajia kuweka jiwe la Msingi katika Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Pangani

Amesema DC Zainab Abdallah

Aidha mkuu wa Wilaya ya Pangani ameomgeza kuwa ziara ya Makamu wa Rais ni pamoja na kutembelea ukuta wa mto Pangani.

kama mnavyofahamu hii miradi ya mazingia iko chini ya Ofisi Makamu wa Rais na kwa bahati mbaya sana mradi huu umejengwa Phase 1 upande huu wa Pangani kwa hiyo bado utekelezaji wa mradi huu kwa Phase 2 kwa maana ya upande wa ng’ambo wa Bweni pamoja na maeneo ambayo yameathirika zaidi kama Pangadeko bado haujatekelezwa kwa hiyo tunaamini ujio wa Makamu wa Rais utaenda kujibu changamoto hizo kwa upande wa utekelezaji wa mradi wa ukuta wa Mto Pangani.

Amesema DC Pangani Bi Zainab Abdallah

Makamu wa Rais anatarajiwa pia kufanya mkutano wa hadhara na Wananchi wa Pangani utakaofanyika katika maeneo ya Bomani Wilayani hapa hivyo Mkuu wa Wilaya amewaomba Wananchi wa Pangani kujitokeza kwa wingi kumsikiliza Makamu wa Rais.

Sikiliza hapa Mkuu wa Wilaya ya Pangani akizungumzia ziara hiyo.