Pangani FM

Mwanafunzi bora wa kijiji aomba msaada kuendelea na masomo Pangani

5 September 2022, 9:21 pm

Mwanafunzi Aisha Ramadhani (20) mkazi wa Kijiji cha Stahabu wilayani Pangani mkoani Tanga ameomba wadau mbalimbali  kumsaidiwa kwa hali na mali ili  ili aweze kumudu kujiunga na masomo ya chuo baada ya kufanikiwa kuhitimu na kufaulu  masomo ya Sekondari.

 

Aisha amemaliza masomo ya sekondari ngazi ya kidato cha 4 katika shule ya Kipumbwi iliyopo wilayani Pangani na kuchaguliwa kusoma chuo cha maendeleo ya jamii kilichopo Mkoani Iringa,nafasi anayoeleza kutamani kuitumia ili kufikia ndoto zake lakini anapata mkwamo kutokana na hali duni ya wazazi wake.

“Baada ya kumaliza  Sekondari kipumbwi Pangani  nimechaguliwa chuo mkoani Iringa, chuo cha maendeleo ya jamii, natamani nisiiache hii nafasi lakini wazazi wangu uwezo hawana, mwenye uwezo anisaidie”-Amesema aisha.

 

Kwa mujibu wa Afisa maendeleo kata ya Mikinguni Bi Matha James mwanafunzi huyo ndiye mwanafunzi wa kike aliyefanya vizuri zaidi katika  kipindi cha miaka 6 aliyohudumu katika eneo hilo.

“tangu nimefika katika kijiji hiki ni miaka takribani 6 imepita sijawahi ona mwanafunzi wa kike amefanya vizuri kijijini hapa Aisha ametuonyesha namna juhudi yake katika masomo imeleta mabadiliko” – Bi Martha

Aisha ameahidi kusoma kwa bidii endapo atapata msaada huo na kuahidi pia kuwasaidia wengine pale atakapofanikiwa kufikia malengo yake

“nikipata  wakunisaidia nitawashukuru, watoe kwa ajili ya Mungu ili sisi ambao hali zetu ziko duni tutoke, tukitoka na sisi ni rahisi kuja kuwanyanyua wengine’’– amesema aisha.

 

Pangani FM pia imezungumza na mama mzazi wa Aisha aliyejitambulisha kwa jina Rukia Bakari ambaye amewaomba wasamaria wema kumuwezesha mwanaye  ili kufanikisha ndoto zake.

“nia yangu mwanangu asome mimi wala baba yake hatuna fedha ya kumpeleka chuo, mwanangu tumemsomesha kwa tabu sana ameridhika na hali yetu akipata hela ya kula anakwenda akikosa hela ya shule anakwenda natamani sema sina uwezo wakumpeleka huko Iringa’’ -Amesema Bi Rukia

 

Mtendaji wa kijiji cha Stahabu  Bw. Mnyamisi Akida amesema kufaulu kwa Aisha ni mafanikio  na imekuwa historia kwao hivyo wanaendelea na jitihada za kumuwezesha kufanikisha ndoto zake.

 ‘’suala la Aisha tumelipokea kwa hali ya juu sana, katika kijiji chetu tuna kamati ya mtakuwa, tumekuwa tukiwaweka kambi na kuhamasisha wanafunzi wasome kwa bidii, ukiangalia wapo Watoto familia zao zina uwezo lakini hawajafanya vizuri kama binti huyu, ukiangalia familia yake ni duni kwetu tunalichukulia ni jambo la mafanikio kwetu’’ – amesema mtendaji wa kijiji Bw. Mnyamisi Akida.