Pangani FM

Polisi Pangani inawashikilia vijana hawa kwa kosa la Kupiga Baruti.

4 January 2021, 1:25 pm

Jeshi la Polisi wilayani Pangani Mkoani Tanga linawashikilia Vijana watatu wakazi wa Pangani Mjini kwa kosa la kupiga Baruti usiku wa kuamkia 1/1/2021 katika eneo la Mnyongeni kwa Mfuga Mbwa

Hayo yamezungumzwa na kamanda wa Polisi wilaya ya Pangani Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Ramadhani Kitanto ambapo amesema kuwa  wanawashikilia vijana  hao na upelelezi ukikamilika watawafikisha mahakamani.

“Kuna vijana watatu walijaribu kupiga mafataki lakini tuliwadhibiti tukawakamata na tunao hivi sasa tunakamilisha uchunguzi tukikamilisha tutawapeleka mahakamani na sasa watakuwa wanaripoti kituoni kila siku mpaka upelelezi ukikamilika tuwapeleke mahakamani.”

Amesema SSP Ramadhani Kitanto

Aidha Kamanda Kitanto ameonya jamii kutojihusisha na masuala ya uhalifu na badala yake kufanya kazi za halali zinazoweza kuwaingizia kipato chao kwakuwa jeshi la polisi limejipanga kulinda usalama wa raia na mali zao.

”Sisi polisi tupo popote kwahiyo kama una tabia ya uhalifu wowote hatutakuacha salama tutakuchukua na sheria itachukua mkondo wake kwahiyo wale wenye tabia za uhalifu waache wafanye kazi kwa njia halali za kujiingizia kipato.”

Amesema SSP Ramadhani Kitanto

Pia kamanda huyo amewaasa wanajamii kuendelea kushirikiana na jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Hayo yamejiri katika mrejesho wa tathimini ya ulinzi na usalama wakati wa sikukuu za Christmas na mwaka mpya wilayani Pangani.