Pangani FM

Ziara ya Waziri Mkuu Tanga: atagawa Mbegu kwa wakulima,Wadau wote wa Mkonge waalikwa kushiriki.

19 January 2021, 4:20 pm

Wadau mbalimbali wa zao la Mkonge Mkoani Tanga wamealikwa kushiriki katika kikao maalum kitakachofanyika Mkoani humo katika Ukumbi wa Regal Naivera Mkoani uliopo Tanga Jiji.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini Kwake.

Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake leo Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela amesema kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu atafanya ziara hiyo kuanzia Tarehe 20 hadi 22 Januari 2021 Mahsusi kwa ajili ya Kufuatilia ufufuaji na uendelezaji wa zao la Mkonge kama moja ya mazao 7 ya Kimkakati ya Kibiashara ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayasimamia kuhakikisha yanafufuliwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kufika na kupokelewa Uwanja wa Ndege Tanga saa 3 Asubuhi moja kwa moja ataenda kutembelea kitalu cha uzalishaji wa mbegu katika Chuo cha utafiti cha Mlingano (Tari-Mlingano) ikiwa ni ufuatiliaji wa maagizo aliyotoa tarehe 1 Juni 2020 alipokuja kwenye kikao maalum kwa ajili ya zao la Mkonge.

Picha ya moja ya matukio katika ziara ya Waziri Mkuu Mkoani Tanga mwezi Juni mwaka 2020.

Baada ya kufika kwenye kitalu atatumia nafasi hiyo kugawa mbegu kwa wakulima wadogo na wakubwa na kuona namna fedha zilizotolewa na Serikali kiasi cha Zaidi ya Tsh Milioni 700 zimetumikaje katika ufufuaji wa zao la Mkonge haswa katika swala zima la mafunzo,utafiti pamoja na uzalishaji wa mbegu na baada ya hapo atakutana na wadau wote wa Zao la Mkonge katika Ukumbi wa Regal Naivera.

Katika kikao hicho atapokea taarifa ya zao la Mkonge katika kipindi chote ambacho Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa agizo namna ambavyo tuliweza kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Kipindi chote ambacho alitoa maagizo si tu kwa Mkoa wa Tanga lakini pia kwa Mikoa mingine inayolima Mkonge kwa maana ya Pwani, Morogoro, Kilimanjaro, Shinyanga, Mara na maeneo mengine ambayo ni wakulima wakubwa wa zao la Mkonge na mara baada ya kupokea taarifa hiyo atapata nafasi ya kuwasikiliza wadau ambao watashiriki kikao hicho na nitumie nafasi hii kuwaalika washiriki wote wakulima, wasindikaji, taasisi za fedha, wafanyabiashra na wengine wanaojihusisha na zao la Mkonge.

Amesema Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Kikao hicho kinatarajiwa kuanza saa 4 Asubuhi na siku Alhamisi tarehe 21 Mheshimiwa Waziri Mkuu atakwenda Wilayani Muheza katika Shamba la Kigombe kwenda kuona shamba la Mkonge.

Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. Magufuli ni serikali ya vitendo kwa hiyo swala la shambani lazma uende shambani na Waziri Mkuu amesema hawezi kuja kuongea na wakulima asiende mashambani kuona uendelezaji wa zao la Mkonge lakini pia baada ya hapo atakwenda kwenye kiwanda kinachosindika mazao yatokanayo na Mkonge ambacho kiko Amboni eneo la Pongwe na baada ya hapo tutakwenda kwenye Ranchi, Ranchi hii kama mnavyofahamu ilikuwa imechukuliwa kinyemela na Kamouni ya Katani na sasa Ranchi hiyo kwa 30% inamilikiwa na Bodi ya Mkonge ambayo ni mali ya Serikali.

Amesema Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Baada ya hapo mheshimiwa Waziri Mkuu atakwenda kuona Shamba la Mkulima Mdogo katika eneo la Magoma, baada ya hapo atamtembelea Mlemavu aliyeibuliwa na Mwandishi wa Habari wa TBC kwa ili kuona hatua iliyifia nyumba ya Mlemavu huyo. Nyumba ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa fedha kwa ajili ya Ujenz wake.

Tarehe 22 Mheshimiwa Waziri Mkuu atakwenda katika wilayani Mkinga kwenye Chuo cha Uhamiaji kinachojengwa Wilayani hapo.

Nyie ni mashahidi wiki hii Waziri wa mambo ya ndani alikuja kufungua mafunzo ya Maafisa wa Idara ya uhamiaji zaidi ya 300 wanaopata mafunzo katika chuo cha Mkinga na kile chuo ndio kinaanza na kinaanza baada ya miaka 17 tangu eneo lilipochukuliwa na Wizara ya Uhamiaji na kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shabiki sana wa kile chuo na alikisema sana wakati wa Kampeni ameelekeza aweze kuona hali ya Chuo na Serikali iweze kuona hatua itakayofanya kwa ajili ya uboreshaji wa Chuo hicho.

Amesema Mkuu wa Mkoa wa Tanga.