Pangani FM

Kivuko cha Pangani kuanza kufanya kazi kwa saa 18

14 December 2022, 9:44 pm

Hatimaye kufuatia hitaji la muda mrefu leo hii Serikali Wilayani Pangani Mkoani Tanga imetangaza kuwa Kivuko cha Pangani-Bweni kimeongezewa muda wa saa 2 za kufanya kazi tofauti na muda wa awali ambapo klikuwa kikifanya kazi kuanzia saa 12 Asubuh mpaka saa Nne usiku hivi sasa muda umesogezwa mpaka saa Sita usiku.

Mbunge wa Jimbo la Pangani Mh. Jumaa Hamidu Aweso pamoja na viongozi wengine katika hafla hiyo

Mbunge wa Jimbo la Pangani Mh. Jumaa Hamidu Aweso pamoja na viongozi wengine katika hafla hiyo

Awali akizungumza kwenye hafla ya kukikabidhi  kivuko cha MV-Tanga kilichokuwa kinafanyiwa ukarabati, mwenyekiti wa halmshauri ya wilaya ya Pangani Akida Bahorera alitoa ombi la kivuko hicho kufanya kazi kwa saa 24.

“wananchi wanatuletea vilio vyao wanaomba Ferry livushe kwa saa 24 kwa sababu huko nyuma kivuko kilikuwa kinavusha kwa saa 24,ila hata ikiwa hadi saa 6 basi wananchi watashukuru”

Katika hotuba yake mkuu wa wilaya ya Pangani Ghaibu Buller Lingo ametoa tamko rasmi la kivuko hicho cha Pangani-Bweni kuwa kuanzia sasa kitafanya shughuli zake hadi saa sita usiku.

“Kivuko hiki kina kamati na mwenyekiti wa kamati hiyo ni mkuu wa wilaya ,hivyo kama mwenyekiti wa kivuko wazo la kufika saa sita kuanzia leo tunapozindua litaanza rasmi”

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba amesema kukamilika kwa kivuko hicho kutaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa wananchi.

‘’Nichukue fursa hii pia kumpongeza mkuu wa wilaya ya Pangani kwa kuchukua maamuzi ya haraka kwa kuongeza muda wa kivuko hichi kutoka saa nne hadi saa sita” aliongeza mkuu huyo wa Mkoa.

Kivuko hiko cha Mv-Tanga  kimekabidhiwa  kuendelea tena na shughuli zake baada ya ukaarabati uliodumu kwa miezi mitatu.

Viongozi walioshiriki katika makabidhiano hayo ni mkuu wa mkoa wa Tanga,akiambatana na viongozi wengine ikiwemo,Naibu Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi na uchukuzi sekta ya Ujenzi,Mbunge wa Jimbo la Pangani,Mkuu wa wilaya ya Pangani na viongozi wengine.