Pangani FM

Wazazi wa Wanafunzi waombwa kufanikisha upatikanaji wa Chakula.

8 February 2021, 1:09 pm

Wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule za msingi wilayani Pangani Mkoani Tanga wameombwa kufanikisha utaratibu wa kambi ya kutwa kwa wanafunzi wa darasa la saba kwa kutoa michango ya chakula katika kambi hizo.

Ombi hilo limetolewa na Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Pangani Bwana Juma Hassan ambapo amewataka wazazi hao kuchangia ili kuwasaidia wanafunzi kupata chakula wanapokuwa shuleni na kuwawezesha kufanya vizuri katika masomo yao.

‘Ili hili liwezekane watoto kukaa kuanzia asubuhi mpaka jioni lazima kuwe na uimarishwaji wa chakula cha wanafunzi asubuhi chai, na chakula cha mchana tukipata hicho kila kitu kitawezekana.’

Amesema Bwana Juma Hassan.

Aidha Afisa huyo amesema idara ya elimu msingi imeweka utaratibu wa kambi za kutwa kwa wanafunzi wa darasa la 7 kuanzia mwezi wa januari 2021 ili kuwawezesha wanafunzi kupata muda mwingi wa kujisomea.

‘Sisi Pangani tumejipanga kuongeza muda badala ya kulala sisi tunasongeza badala ya wao darasa la saba kuanza vipi saa mbili kamili tukasema waanze saa moja kamili asubuhi mpaka saa kumi na moja kwa shule zenye watoto wanaotembea umbali mrefu na saa kumi na mbili kwa shule za mjini kama kutakuwa na ulazima wa kulala mimi na timu yangu tutapita na kukagua mazingira kama yanaridhisha.’

Amesema Bwana Juma

Utaratibu wa kuwaweka kambi wanafunzi wa madarasa au vidato vyenye Mitihani ya Kitaifa ni miongoni mwa hatua za ubunifu zilizofanywa na baadhi ya Shule ili kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani