Pangani FM
Pangani FM
6 June 2024, 11:10

Upo umuhimu mkubwa kwa jamii hasa vijana kuelewa na kushriki katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Na Majabu Madiwa
Wilaya ya Pangani imeanzisha kampeni maalum ya usafi itakayoshindanisha vitongoji ili kuimarisha hali ya usafi katika wilaya hiyo.
Hayo yamejiri ikiwa dunia inaadhimisha kilele cha siku ya mazingira inayoadhimishwa Juni 5 kila mwaka ambapo katika wilaya ya Pangani maadhimisho hayo yamefanyika kwa shughuli za ufanyaji wa usafi katika hospitali ya wilaya ya Pangani.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ambaye ni Afisa tarafa ya Pangani Mjini Bi Heliswida Simon Majura amewataka wananchi wa vitongoji hivyo kushirikiana na viongozi wao wa vijiji ili kufanikisha kampeni hiyo.
Akitoa salamu za Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bw. Musa Kilakala, afisa tarafa huyo amewasisitiza wanapangani kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao kila siku kwani usafi wa mazingira ni suala endelevu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Bw. Ramadhan Zuber akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, amewaelekeza wataalam wa idara ya misitu na mazingira kuingia kwenyemichakato ya biashara ya hewa ukaa ili halmashauri ijipatie kipato sambamba na kuongeza shughuli za utunzaji wa misitu.
Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani mwaka huu yamepambwa na kauli mbiu isemayo; Urejeshwaji wa ardhi na ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame.