Pangani FM

Mama ajifungua Watoto Mapacha Watatu Pangani

7 January 2021, 9:16 am

Mwanamke  mmoja mkazi wa kijiji cha Kwakibuyu Wilayani Pangani Mkoani Tanga amejifungua watoto mapacha watatu siku ya  Januari Mosi 2021.

Pangani FM imemfikia Mwanamke huyo na kufanya naye mahojiano akiwa katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Wilaya ya Pangani.

Licha ya kueleza furaha yake ya kupata mapacha watatu wote wakiume Mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la MANJAA HASANI amewaomba wadau kumsaidia katika kuwahudumia watoto wake hasa katika kipindi hiki cha awali ambacho watoto wao wanatakiwa kupata maziwa ya kutosha.

“Huu ni uzazi wangu wa Tano hivyo sasa nina watoto Saba , Baba watoto amepokea vizuri taarifa hizi ila isipokuwa ndio hivyo Uchumi.. kumudu kuwanyonyesha watoto wote  watatu siwezi,ila kama ndio sina jinsi itabidi niwalee sababu ni wanangu”

Amesema Bi. Manjaa

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Pangani Dkt HASANI MSAFIRI amet hibitisha mama huyo kujifungua watoto mapacha watatu na wanaendelea vizuri ikiwa bado wako kwenye uangalizi katika hospitali hiyo.

Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii Wilaya ya Pangani BW TADEI KUSAI KAMISA ameeleza jitihada walizofanya ili kumsaidia Mama huyo na Mapacha waliozaliwa katika upatikanaji wa mahitaji muhimu.

“Ni jambo pia la Kumshukuru Mungu kwamba Mama amejifungua watoto watatu lakini kimsingi suala lililopo mbele yetu ni kumsaidia, tumefanikiwa kumpata mdau mmoja toka Tanga ambaye anaendesha Shirika linaitwa Pamoja Leo ambalo limekuwa likitoa huduma kwa watoto wanaopata ugumu wa kunyonya maziwa ya Mamam kwa hiyo huyo mdau amekuja na huyu Mamam amefanikiwa kupata msaada wa kupatiwa maziwa, vifaa vya kuzimulia maziwa, vifaa vya kubebea watoto na watoto wake wameingia kwenye utaratibu wa kulelewa kwa kupewa lishe ya Maziwa kwa muda wa Mwaka mmoja kwa hiyo kila Alhamisi huyu Mama itabidi awe anaenda Clinic ya shirika hilo iliyopo  Tanga Mjini”

Amesema Bwana Tadei

Aidha Bw Tadei amesema mama huyo anahitaji msaada wa kiutu huku akiwataka wadau kuguswa na kumsaidia mama huyo na watoto wake.

“Kimsingi hana uwezo watoto watapata Formula Milk lakini pia watahitaji kunyonya Mama atahitaji awe na Afya nzuri mpe chochote ulicho nacho guswa moyoni katoe msaada kwa Yule Mama”

Amesema Bwana Tadei.