Pangani FM

Wakulima Pangani wanavyotumia redio kustahimili mabadiliko ya tabianchi

30 January 2023, 12:29 pm

Martine Nekwa, Mkulima wilayani Pangani anayetumia Redio Kustahimili Mabadiliko ya tabianchi. Picha na Erick Mallya.

Mabadiliko ya tabianchi yameleta changamoto nyingi katika mifumo ya uzalishaji na hata maisha ya kila siku. Hali hii inafanya upatikanaji wa taarifa na huduma za  hali ya hewa kuwa suala la msingi na la dharura.

Na Erick Mallya

Wataalamu wamethibitisha kuwa kurahisihishwa kwa usambazwaji na upatikanaji wa taarifa pamoja na huduma za hali ya hewa kwa sekta nyeti kama vile ya kilimo kutaiwezesha jamii kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kustahimili mabadilko ya tabianchi.

UZIKWASA kupitia Pangani FM imekuwa mstari wa mbele  katika kuwezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za hali ya hewa wilayani Pangani kwa kurusha taarifa za kila siku kutoka mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA).

Taarifa hizi ni kama vile muelekeo wa misimu ya mvua, angalizo ushauri na tahadhari za mapema.

Redio Pangani pia ina kipengele  maalum  kila siku kwa ajili ya taarifa za hali ya hewa.

Kupitia kipindi chake maalumu cha nitunze-nikutunze kinachoruka kila siku ya Ijumaa kuanzia saa 12:30 jioni mpaka saa 2:00 Usiku Pangani FM huwashirikisha wataalam wa hali ya hewa na sekta zinazoingiliana kutoa maelezo ya kina kwa jamii kuhusu msimu husika, utabiri wa vipndi vjavyo na nini kifanyike ili kustahimili.

Kipindi hicho huta fursa pia kwa wasikilizaji  kupiga simu moja kwa moja Studio na kuuliza maswali yao kwa  wataalamu waliopo Studio.  

Hayo huwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi juu ya aina ya mazao ya kupanda kwenye msimu husika au yapi ya kuyapa kipaumbele.

“Wakulima wanatakiwa kuelimishwa vyema kuhusu taarifa za hali ya hewa ili waweze kujiandaa na kuamua nini cha kufanya, nini cha kupanda na nini cha kuacha kulingana na msimu husika. Kipindi hiki kina manufaa makubwa kwa wakulima wa hapa Pangani wito wangu ni kwamba wakulima wasikilize Pangani FM kwa sababu kama watafuatilia basi kitawanufaisha sana haswa zama hizi za mabadiliko ya tabianchi.”

Amesema Martine Nekwa Mkulima katika kijiji cha Tungamaa wilayani Pangani

Sauti ya Mkulima Martine Nekwa mkazi wa Pangani anayenufaka na Redio kwenye Kilmo.

Sekta nyingine zizonanufaika na huduma za hali ya hewa kupitia UZIKWASA/Pangani FM ni pamoja na ufugaji,uvuvi, maliasili, utalii na wanyamapori, nishati,maji, usafiri wa baharini, na mamlaka za usimamizi wa  afya na maafa.

Pamoja na jitihada hii UZIKWASA inatarajia kuanza kuzijengea uwezo kamati za usimamizi wa rasilimali bahari (BMU) pamoja na  za mazingira kuongeza nguvu katika kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Kufanikisha hivyo UZIKWASA itazipatia mafunzo ya uongozi wa mguso ili kuziwezeshwa kutengeneza mipango kazi rafiki na yenye tija zaidi katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.