Boma Hai FM

Milioni 33.4 kuboresha vyoo Romu

28 September 2026, 7:42 am

Pichani ni Diwani wa kata ya Romu Salim Mfoy akizungumza na wananchi pamoja na kamati ya shule wakati wa mapokezi ya fedha za ujenzi wa choo (Picha na Juma Robert)

“Tushirikiane kusimamia ujenzi huu ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.”– Salim Mfoy Diwani wa Kata ya Romu

Na Juma Robert

Hai -Kilimanjaro

Diwani wa Kata ya Romu wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro Salim Mfoy, ameishukuru serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 33.4 kwa ajili ya ujenzi wa matundu mapya ya vyoo katika shule  za msingi  Kishare na Kitifu, akisema mradi huo utasaidia kuboresha mazingira ya usafi na kujifunzia kwa wanafunzi.

Sauti ya Salim Mfoy, Diwani wa kata ya Romu

Mfoy ameyasema hayo Septemba 24 2026, wakati wa utambulisho wa mradi huo, ambapo amewataka wananchi na uongozi wa shule kushirikiana katika usimamizi wa ujenzi ili ukamilike kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Amesema uwepo wa vyoo bora shuleni ni sehemu muhimu ya kulinda afya za wanafunzi na kuwawezesha kupata mazingira salama na rafiki wakati wa masomo.

Kwa upande wake mwalimu wa shule  ya msingi  Kitifu Rebecca Sevelin, amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutawasaidia wanafunzi kupata mazingira salama ya kujisaidia na kuimarisha usafi wa mazingira shuleni.

Pichani ni Rebecca Sevelin Mwalimu wa shule ya msingi Kitifu akizungumzia mapokezi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo(Picha na Juma Robert)
Sauti ya Rebecca Sevelin Mwalimu wa shule ya msingi Kitifu

Naye mwananchi wa Kata ya Romu Hassan Meena ameishukuru Serikali kwa kupeleka fedha hizo, huku akiwataka wananchi kushirikiana na viongozi katika kusimamia ujenzi na kutunza miundombinu hiyo baada ya kukamilika.

Pichani ni Hassan Meena mwananchi wa Kata ya Romu akizungumzia mapokezi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo(Picha na Juma Robert)
Sauti ya Hassan Meena mwananchi wa Kata ya Romu