Boma Hai FM

Viongozi wa vijiji Hai wahimizwa kuwatambua wanaotoa tiba asili

11 July 2026, 4:43 pm

Pichani ni Mwenyekiti wa mamlaka ya Mji mdogo Wilaya ya Hai Julius Swai (katikati) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Mhe. Edmund Rutaraka( Kulia) pamoja na Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Hai Ndg. Zephania Gunda ( kushoto) (Picha na Juma Robert)

Viongozi wa Vijiji na mitaa wilaya ya Hai wameashwa kuwatambua watu wote wanaotoa tiba asili, kufuatia vifo vya watu wanne wa familia moja waliofariki kwa kudhaniwa wamekunywa dawa za asili.

Na Oliver Joel

Mwenyekiti wa Mji Mdogo Bomang’ombe, Julius Swai, amewataka viongozi wa vijiji na mitaa kuhakikisha wanawatambua watu wote wanaojihusisha na utoaji wa tiba asili katika maeneo yao ili kuzuia madhara yanayoweza kuwapata wananchi kutokana na matumizi ya dawa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika.

Swai ametoa wito huo leo, Julai 10, 2026, wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Mji Mdogo Bomang’ombe kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Amesema hatua hiyo ni muhimu hasa baada ya kupita siku moja tangu watu wanne wafariki dunia katika tukio linalodhaniwa kuhusishwa na matumizi ya dawa za asili ambazo hazikuwa zimethibitishwa na mamlaka zinazohusika.

Sauti ya Mwenyekiti wa Mji Mdogo Bomang’ombe, Julius Swai

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, amesema mafanikio ya wilaya kupata hati safi hivi karibuni yanatokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na uwajibikaji wa viongozi kuanzia ngazi ya vijiji.

Rutaraka amewapongeza viongozi na watendaji kwa ushirikiano wao na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kudumisha uwazi, uwajibikaji na kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Hai.
ushirikiano huo ndio msingi wa kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na wananchi wanaendelea kunufaika na huduma bora zinazotolewa na serikali.