Boma Hai FM
Boma Hai FM
20 May 2026, 11:27 am

Katika maadhimisho ya siku ya nyuki duniani wafugaji wa nyuki wametakiwa kuhifadhi asali katika vifungashio salama na sio chupa zilizoisha vinywaji.
Na Oliver Joel, Hai- Kilimanjaro
Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya nyuki duniani yatakayofanyika kesho, wafugaji nyuki wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuhifadhi asali katika vifungashio salama badala ya kufungasha katika vyombo vilivyoisha vinywaji ambavyo vinaathiri ubora wa asali.
Wito huo umetolewa May 19 2026, na afisa nyuki wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Beatrice Mlelwa wakati alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu ya radio Boma Hai Fm
Amesema kuwa kuhifadhi asali katika vifaa hivyo kuna athiri ubora wa asali kwa kuwa asali ina tabia ya kufyonza harufu kwa uraisi hivyo itakapowekwa katika chupa hizo itafyonza harufu ya chupa hiyo na kuharibu ubora wake,hivyo amewataka wafugaji kutumia vifungashio vipya ambavyo havijawekwa bidhaa nyingine ili kutunza ubora wa asali.
Naye Edward Kitenyi ambaye pia ni afisa maliasili wilayani Hai amesema kuwa awali ufugaji nyuki ilikuwa ni shughuli iliyokuwa inafanywa na wazee pekee ila kwa sasa udugaji nyuki unafanywa na vijana na hata kina mama pia kwani ni shughuli yenye gharama nafuu na inayokuza kipato cha familia na mtu mmoja mmoja.
Akizungumzia mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa ufugaji nyuki Erick Mrema ambaye ni afisa nyuki wilaya ya Hai amesema kuwa matumizi ya viuatilifu vyenye sumu vinavyotumika mashambani wakati wa kilimo vina athari kwa nyuki wakati wanapofanya uchavushaji katika mimea hiyo,hivyo amewataka wakulima kutumia viuatilifu ambavyo ni salama kwa nyuki .
Maadhimisho ya siku ya nyuki duniani hufanyika kila mwaka ifikapo may 20,ambapo mwaka huu kauli mbiu ni”uhifadhi wa nyuki kwa ustawi wa mazingira na Taifa letu”.