Boma Hai FM

Wanawake waomba kujengewa kituo cha kulelea watoto kazini

12 March 2024, 2:06 pm

Mkurugenzi Mtendaji KCMC na mtendaji wa Shirika la Msamaria mwema Prof. Gileard Masenga aliyevaa shati la kitenge akiingia ukumbini wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Kuringe,manispaa ya Moshi (Picha na Janeth Joseph)
Wanawake watumishi kutoka taasisi mbalimbali kutoka taasisi mbalimbali wakifurahia katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani (Picha na Janeth Joseph)

Kutokana na changamoto za malezi ya watoto zinazowakabili wanawake watumishi katika taasisi mbalimbali, watumishi hao wameomba kujengewa kituo cha kulelea watoto.

Na Elizabeth Mafie

Wanawake watumishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kupitia shirika lake la  Msamaria Mwema(GSF) wameomba kuwekewa mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa kujengewa  kituo  maalum cha kulelea watoto wao pindi wanapomaliza likizo ya uzazi  ili waweze kuwa karibu na watoto wao wawapo kazini kwa  kupata muda wa kunyonyesha watoto wao badala ya kurudi nyumbani mchana kunyonyesha.

Wamesema baada ya likizo ya miezi mitatu kuisha wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali za usafiri hasa wanapotakiwa kurudi nyumbani mchana kunyonyesha watoto na kwamba muda wa kwenda na kurudi hautoshi hivyo kufanya kazi katika mazingira magumu.

Sauti ya Mkuu wa Idara rasilimali watu KCMC Dorah Olotu

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa hospitali ya KCMC Dorah Olotu mbele ya Katibu Mkuu Mtendaji wa Shirika hilo na  Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya KCMC Profesa Gileard Masenga wakati wa  kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo yamefanyika jana katika ukumbi wa Kuringe, Manispaa ya Moshi.

Olotu amesema kuwa  shirika hilo lina wanawake zaidi ya 1,118 ambao  umri wao bado ni kwa kuzaa hivyo akaliomba shirika hilo kuona umuhimu wa kujenga kituo maalum kwa ajili ya watoto wao ili pindi wanapotaka kwenda kunyonyesha iwe ni rahisi.

Ameongeza kuwa  wazo la serikali la mama kutoka kazini saa saba na  kwenda kunyonyesha mtoto wake linakuwa halifanikiwi,  na wameona  ni changamoto na ni kilio cha wanawake wengi kutokana na wasichana wanaowasaidia kulea watoto hao baadhi yao hutoroka na wengine huondoka kwa kushtukiza huku mwanamke huyo akitakiwa kwenda kazini.

Ameeleza kuwa kuna changamoto nyingi ambazo zinahusiana na malezi ya watoto, hivyo kama Katibu Mtendaji wa shirika la Msamaria Mwema akiwajengea kituo cha kulelea watoto, watoto wao watapata  huduma nzuri na kwamba  wafanyakazi watatulia kazini, na kufanya  kazi kwa bidii pamoja na kuongeza ufanisi huku watoto wakiendelea kuwa na afya njema.

Akijibu ombi la wanawake hao, Prof. Masenga amesema kuwa lipo eneo ambalo lilitengwa na shirika hilo hivyo wataangalia namna ya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho maalum kwa ajili ya watumishi wanawake wa shirika hilo.

Sauti ya mkurugenzi mtendaji KCMC na mtendaji wa shirika la Msamaria Mwema Profesa Gileard Masenga.