Boma Hai FM
Boma Hai FM
20 May 2026, 4:34 pm

Katika kuendelea kutunza mazingira wananchi wa kijiji cha Kwasadala wameweka maazimio ya kuweka kijiji hicho katika hali ya usafi na kukubaliana kuweka faini kwa yeyote atakaekaidi.
Na Elizabeth Mafie
Hai- Kilimanjaro
Wananchi wa Kijiji cha Kwasadala wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wamekubaliana kwa pamoja kuweka faini ya shilingi 30,000 kwa mwananchi yeyote atakayekutwa akitupa taka ovyo au kukaidi kushiriki shughuli za usafi zinazofanyika kila Alhamisi ya mwisho wa mwezi.

Makubaliano hayo yameafikiwa Mei 20, 2026 katika mkutano wa robo ya tatu wa kijiji hicho uliofanyika katika ofisi ya kijiji.

Mkutano huo ulihudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi, ukiwa na ajenda kuu za kusoma taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji, kubadilisha matumizi ya ardhi kwa ajili ya kupata eneo la kujenga shule ya sekondari, pamoja na kuweka mikakati ya kudhibiti hali ya uchafu katika kijiji cha Kwasadala.
Kupitia mkutano huo, wananchi walipitisha maazimio muhimu ambayo yanatarajiwa kuleta maendeleo makubwa katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa furaha baada ya mkutano huo, wananchi wa Kwasadala wamesema kuwa uamuzi wa kubadilisha matumizi ya ardhi iliyopo chini ya wizara ya mifugo na kilimo ili kupisha ujenzi wa shule ya sekondari utasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.
Kwa mujibu wa wananchi hao, hali hiyo imekuwa ikiwasababishia wanafunzi kukumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo uchovu na hatari za njiani.

Wananchi pia wameeleza kuwa kwa muda mrefu eneo la Kwasadala limekuwa likikumbwa na tatizo la uchafuzi wa mazingira kutokana na baadhi ya wakazi kutupa taka hovyo na wengine kushindwa kushiriki shughuli za usafi wa mazingira.
Wamesema kuwa uwekaji wa faini hiyo ya shilingi 30,000 utasaidia kurejesha nidhamu na kuhakikisha kijiji kinakuwa safi wakati wote.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Kwasadala Edwine Lamtey, amesema kuwa kijiji hicho kina utaratibu wa kufanya mikutano ya mara kwa mara kwa lengo la kuwapa wananchi taarifa za mapato na matumizi pamoja na kuweka mikakati ya maendeleo.
Amesema kuwa katika mkutano huo, wananchi wameazimia kubadilisha matumizi ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari na kuweka faini kwa wote watakaobainika kutupa taka hovyo.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwasadala Issa Nassor amesema kuwa mkutano huo ulikuwa wa kipekee kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi na mwamko wao wa kushiriki katika maendeleo ya kijiji.
Ameeleza kuwa kwa kuwa maamuzi hayo yametokana na wananchi wenyewe, utekelezaji wake unatarajiwa kwenda vizuri bila vikwazo.