Boma Hai FM

Polisi Bomang’ombe watoa wito kwa wazazi kulea watoto wao

27 July 2026, 1:32 pm

Pichani ni askari wa Jeshi la polisi Bomangombe wakiwa na baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo cha Neema Orphanage Center baada ya kukabidhi zawadi na mahitaji kwa watoto hao (Picha na Henry Keto)

Jeshi la polisi wilaya ya Hai limetembelea kituo cha kulea watotot yatima cha Neema Orphanage Center na kutoa wito kwa wazazi kulea watoto wao.

Na Henry Keto,Hai-Kilimanjaro

Jeshi la Polisi Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro limewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kulea na kuwalea watoto wao ili kupunguza tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Wito huo umetolewa Julai 25, 2026 na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Hai (Bomang’ombe), Assp Suzan Kidiku, wakati wa ziara ya askari wa jeshi hilo katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Neema Orphanage Center kilichopo Kata ya Machame Kaskazini, ambapo wamekabidhi mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo.

Assp Kidiku amesema misaada hiyo imetolewa na askari wapya wa kundi la K3 kama sehemu ya kutoa shukrani kwa Mungu baada ya kufanikiwa kuajiriwa, wakiamini kuwa ni muhimu kushirikisha baraka walizozipata na watoto wenye uhitaji.

Amesema hatua hiyo pia inalenga kuhamasisha jamii kuendelea kuwajali watoto wanaoishi katika mazingira magumu badala ya kuwaacha wakikosa malezi na kujikuta wakiingia mitaani.

Sauti ya Afande OCD-Hai ASSP- Suzan Kidiku

Naye Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Hai, SP Elishafra Kilavo amewapongeza askari hao kwa moyo wa kujitolea, akisema matendo ya kuwasaidia wenye uhitaji yanaimarisha mshikamano na kuonyesha kuwa Jeshi la Polisi lina wajibu wa kushiriki shughuli za kijamii pamoja na kulinda usalama

Sauti ya Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Hai, SP Elishafra Kilavo

Kwa upande wake Afande INSP Abdulrazak Mtota amesema kitendo cha askari hao kutoa sehemu ya kipato chao kuwasaidia watoto yatima ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na jamii, kwani kinawapa watoto hao faraja, matumaini na tabasamu.

Sauti ya Mkaguzi kata ya Machame Mashariki Afande INSP Abdulrazak Mtota
Pichani ni Askari wapya namba K3 walioajiriwa hivi karibuni wakiwa kwenye ukimbi wa Neema Orphanage Center kuwatembelea watoto wanaolelewa hapo (Picha na Henry Keto

Akizungumza kwa niaba ya kituo hicho Msimamizi wa Neema Orphanage Center, Sister Anna Kiluswa, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo na kusema umeonyesha upendo wa kweli kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo huku akiwaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia makundi yenye uhitaji.

S auti ya Msimamizi wa Neema Orphanage Center, Sister Anna Kiluswa
Pichani ni Askari wapya namba K3 wakiwa na baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo cha Neema Orphanage Center (Picha na Henry Keto)

Neema Orphanage Center kinahudumia watoto 54 wenye umri wa kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 21 na Kati yao, watoto wa kike ni 25 na wa kiume ni 29, huku baadhi yao wakiwa wanaendelea na masomo katika shule za bweni na vyuo mbalimbali.