Boma Hai FM
Boma Hai FM
27 August 2026, 11:58 pm

Wafanyabiashara wadogo marufu machinga na wale wote wenye mitaji kuanzia sifuri hadi milion 4 wilaya ya Hai mbioni kupata ofisi inayojengwa kwa zaidi ya milioni 43.
Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro
Katibu Mkuu wa Wafanyabiashara Ndogondogo Mkoa wa Kilimanjaro, Willy Stivin Kavishe, amesema kukamilika kwa ujenzi wa jengo jipya la ofisi ya wafanyabiashara wadogowadogo Wilaya ya Hai kutawawezesha wafanyabiashara kupata sehemu rasmi ya kukutana, kubadilishana mawazo na kupata taarifa sahihi kuhusu fursa mbalimbali za biashara.
Kavishe ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo linalojengwa ndani ya Soko la Gezaulole, Mjini Bomang’ombe, Wilaya ya Hai, akiwa ameambatana na Sekretarieti ya Mkoa ya Wafanyabiashara Ndogondogo.
Amesema jengo hilo linajengwa kwa fedha za Serikali, hatua ambayo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwawezesha wafanyabiashara wadogo katika maeneo mbalimbali

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wamachinga Tanzania Wilaya ya Hai, Paul Malongo, amesema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia wafanyabiashara kuwa na eneo rasmi la kuwasilisha changamoto na kero zao kwa viongozi, ili ziweze kufikishwa serikalini na kutafutiwa ufumbuzi.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi milioni 43,690,400 hadi kukamilika kwake.