Boma Hai FM
Boma Hai FM
3 September 2026, 11:52 am

Mkuu wa Wilaya ya Hai Hassan Bomboko amesisitiza ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kufungua mitaro na njia za maji, huku akiwataka wakazi wa maeneo hatarishi kuchukua tahadhari mapema kwa kuhama kwa muda na kulinda mali zao dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za Elnino zinazotarajiwa kunyesha hapa nchini.
Na Richard Salema & Gervas Mosha
Hai – Kilimanjaro
Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Hassan Bomboko, amezitaka mamlaka na wananchi kuchukua tahadhari na hatua za haraka kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha, ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana mvua hizo za El Nino.
Bomboko ameyasema hayo Agosti 31 2026, wakati wa ziara ya kukagua maeneo yenye changamoto pindi mvua zinaponyesha katika kata za Muungano, Bomang’ombe na Bondeni wilayani Hai.

Amesema hatua hizo zinapaswa kuhusisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari dhidi ya mvua, pamoja na ushirikiano kati ya mamlaka na wananchi katika kufungua mitaro na njia za maji ili kuzuia maji kutuama na kuingia katika makazi huku akiwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama kwa muda,pamoja na kuhamisha mifugo na vitu vinavyoweza kuharibika ili kuepusha hasara.
Aidha amemtaka Meneja wa TARURA kushirikiana na wananchi katika kutengeneza mitaro na njia za maji, huku viongozi wa mji mdogo, kata, vijiji na vitongoji wakihakikisha njia za maji zinafunguliwa kutoka yanapotokea hadi yanapoishia.
Kwa upande wao, wananchi wameomba hatua zichukuliwe kukabiliana na changamoto zinazochangia maji kuingia katika makazi , huku mkazi wa Gezaulole, Japhet Urasa,akiishauri serikali kushughulikia makazi yaliyojengwa katika maeneo yanayozuia njia za maji.

Naye Hilda Mushi amewataka wananchi kushirikiana kufanya usafi na kuboresha mazingira, hususan kufungua njia za maji, ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha.
Bomboko amesema serikali itaendelea kufuatilia hali hiyo na kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unalindwa, huku akisisitiza kuwa endapo miundombinu itaathiriwa, hatua zichukuliwe kuhakikisha wanafunzi wanapata maeneo salama ya kuendelea na masomo.