Boma Hai FM

Mbunge Saashisha Mafuwe amlilia katibu wake

6 January 2024, 10:21 pm

kulia ni mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe akiweka shada la maua pamoja na mbunge wa jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo katika kaburi la katibu wa mbunge wa jimbo la Hai mwalimu Benson Lema (picha na Elizabeth Mafie)

Aliyekuwa katibu wa mbunge jimbo la Hai Mwl. Benson Lema azikwa kijijini kwao Nronga – Machame.

Na Elizabeth Mafie

Mamia ya waombolezaji wakiongozwa na mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe wameshiriki katika ibada ya maziko ya aliyekuwa katibu wake  na mwalimu mstaafu Benson Lema aliyeaga dunia  januari 2 2024 katika hospitali ya Machame  huku wakimzungumzia kama mpenda maendeleo na mtu aliyejitoa katika jamii.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuuaga mwili wa marehemu Mwalimu  Benson Lema mbunge wa jimbo la Hai Saashisha mafuwe amesema kuwa Mwl Benson Lema alikuwa kiungo mkubwa katika jamii na moja ya mtu aliyependa kujishusha na kuwa mfano wa kuigwa katika kila nafasi aliyotumika huku akimwelezea kama nguzo ya mtu aliyesimama katika mstari bora wa maadili na uongozi.

Saashisha amesema kuwa maisha ya Mwalimu Benson Lema yamefanyika baraka kwa jamii yake na kwamba ni wazee wachache wanaopenda jamii yao kwa dhati  kwani katibu huyo alikuwa mwadilifu wa kweli na mtu asiyependa mzaa hasa katika utendaji wake wa kazi.

Sauti ya mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe.

Akizungumza wakati wa ibada ya maziko ya Mwalimu Benson Lema  yaliyofanyika hii leo katika usharika wa Nronga  Machame  Mchungaji  Calvin Kessy   wa usharika wa Uswaa aliyemwakilisha mkuu wa jimbo la Hai amesema kuwa Mwalimu  Benson Lema aliishi maisha yenye maadili ambapo vijana wengi wa sasa wanashindwa kuyaishi hasa pale wanapoishi maisha ya kubweteka na kuwa tegemezi kwa wazazi wao.

Kwa upande wao baadhi ya waombolezaji  waliotoa salamu za rambirambi wamemzungumzia mwalimu Benson Lema kama mmoja wa mtu aliyependa kutengeneza viongozi katika jamii huku akijitoa katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya  mkuu wa wilaya ya Hai katibu tawala wa wilaya ya Hai Sospeter Magonera amesema kuwa wilaya imepoteza mchapa kazi na mpenda maendeleo na kwamba alikuwa na busara na hekima na msaada kwa watu wengi.

Sauti ya katibu tawala wilaya ya Hai Sospeter Magonera.

Mwalimu Benson Lema alistaafu rasmi kazi ya ualimu mwaka 2014 na kisha mwaka 2020 mbunge Saashisha Mafuwe alimuomba awe katibu wake, kazi aliyoifanya hadi umauti ulipomfika. BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.