Boma Hai FM
Boma Hai FM
22 July 2026, 11:03 am

Wananchi wa Wilaya ya Hai wameitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kuviamini vyombo vya dola, wakisisitiza kuwa kuheshimu utawala wa sheria ni njia sahihi ya kuhakikisha haki inatendeka.
Na Bahati Chume
Hai- Kilimanjaro
Wananchi wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wameonya dhidi ya tabia ya kujichukulia sheria mkononi, wakisema vitendo hivyo vinakiuka haki za binadamu na vinaweza kusababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha.
Wito huo umetolewa kufuatia tukio la Julai 18, 2026, ambapo kijana aliyefahamika kwa jina la Felex Kileo mkazi wa Gezaulole, Bomang’ombe, alidaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana na kuchomwa moto hadi kufariki dunia katika eneo la Zarau, kijiji cha Mkombozi, wilayani Hai. Inadaiwa alikuwa akihusishwa na mtandao wa wizi wa maguta na pikipiki.
Wakizungumza na waandishi wa habari Julai 20, 2026 baadhi ya wananchi Wamesema kitendo hicho hakikubaliki katika jamii inayozingatia utawala wa sheria, wakisisitiza kuwa kosa la kuua ni jinai na linakiuka haki za msingi za binadamu.
Mmoja wa wananchi hao Kassimu Juma wa Bomang’ombe, amesema ni muhimu wananchi wakumbuke kuwa Tanzania inaongozwa kwa mujibu wa sheria, hivyo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kutoa adhabu kwa kujichukulia sheria mkononi.
Felex Kileo alizikwa Julai 20, 2026, nyumbani kwao katika kijiji cha Samaki Maini, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa, amedhibitisha kupokea taarifa za tukio hilo, akisema mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umechomwa moto na kwamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika.