Boma Hai FM

Diwani Njau afungua mafunzo atoa wito kwa wajasiriamali kulinda mitaji na vipato

22 May 2026, 9:10 am

Pichani ni Diwani wa kata ya Bomang’ombe Mhe. Evodi Fidelisi Njau wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wajasiriamali (Picha na Henry Keto)

Wajasiriamali wa kata ya Bomang’ombe wamepatiwa mafunzo maalumu ya kulinda mitaji yao na vipato vyao pamoja na kuanzisha biashara kwa mitaji midogo, wamefundishwa kutengeneza batiki, sabuni ushonaji na mafunzo mengine ya ujasiriamali.

Na Henry keto, Hai-Kilimanjaro

Diwani wa Kata ya Bomang’ombe, Mhe. Evodi Njau, amefungua rasmi mafunzo ya ujasiriamali yanayowezeshwa na Chuo cha Mafunzo Maalumu, huku akitoa wito kwa wajasiriamali kutumia fursa hiyo kuimarisha maisha yao kwa kulinda vipato na kuanzisha mitaji mipya.

‎Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo May 21,2026 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Klasta uliopo Shule ya Msingi kibaoni Kata ya Bomang’ombe, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Mhe. Njau amesema wajasiriamali wanapaswa kufanya biashara kwa ujasiri bila kuogopa changamoto za ufinyu wa mitaji au kuwategemea watu wengine.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Bomang’ombe Mhe. Evodi Njau.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Kata ya Bomang’ombe, Joyce Masawe, amewapongeza wananchi waliojitokeza kushiriki mafunzo hayo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa kata hiyo.

‎Masawe alisema mafunzo hayo yana mchango mkubwa kwa jamii kwani huwajengea uwezo wa kujiajiri, kuongeza kipato na kuwapatia fursa ya kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali bila riba

Sauti ya Afisa Maendeleo kata ya Bomang’ombe Joyce Masawe
Pichani ni Wajasiriamali waliojitokeza kwenye mafunzo ya ujasiriamali kata ya Bomang’ombe Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro (Picha na Henry Keto)

Naye Mkufunzi Mkuu wa mafunzo hayo Saravai Rashid Izina amesema kuwa mafunzo ya siku tatu yatawasaidia washiriki kutambua fursa mbalimbali za biashara na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

‎Alisema kuwa maarifa yatakayotolewa yatawasaidia wajasiriamali kuondokana na umasikini, akisisitiza kuwa mtaji unaweza kuanzia kwenye rasilimali ndogo zilizopo mikononi mwao.

Sauti ya Mkufunzi Mkuu wa mafunzo hayo Saravai Rashid Izina

Pichani ni Mkufunzi Mkuu (Katikati) akitoa mafunzo namna yakutengeneza batiki za kuchapa (Picha na Henry Keto)

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamemshukuru Diwani wa Kata ya Bomang’ombe kwa kuona umuhimu wa kuwawezesha wajasiriamali, wakisema elimu hiyo itawasaidia kuongeza ujuzi, kuboresha mitaji yao na kufanya biashara hata kwa mtaji mdogo.

‎Washiriki hao walieleza matumaini yao kuwa mafunzo hayo yatakuwa mwanzo wa mabadiliko chanya katika shughuli zao za kiuchumi na kuinua vipato vya familia zao

Sauti za washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali.