Boma Hai FM

Wananchi, wanafunzi wapatiwe elimu ya lishe bora-DC Bomboko

2 February 2026, 12:16 pm

Pichani ni Mkuu wa wilaya ya Hai Mhe. Hassan Bomboko (katikati) pamoja na katibu tawala wa wilaya Sospeter Magonera(kushoto), na kaimu mkurugenzi wilaya ya Hai Bakarani Urio(kulia) pamoja na Mganga mkuu wa wilaya ya Hai Dr.Itikija Msuya.

Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Hai imefanya kikao cha robo kwaajili yakutathmini hali ya lishe na upatikanaji wake katika kata kumi na saba za wilaya ya Hai zikihusisha wataalamu wa lishe pamoja na maafisa watendaji wa kata.

Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro

Mganga Mkuu wa wilaya ya Hai, Dkt. Itikija Msuya amewataka wananchi kubadilisha mtindo wa maisha na kuacha ulaji holela, kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na lishe ili kujenga afya bora na kuzuia magonjwa yatokanayo na lishe duni.

Dkt. Itikija amesema kufuata misingi ya lishe bora ni hatua muhimu katika kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, huku akisisitiza wananchi kujitokeza kupata elimu ya lishe kutoka kwa wahudumu wa afya waliopo maeneo yao.

Akizungumza Januari 30, 2026, wakati wa kikao cha lishe kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa wilaya ya Hai, Dkt. Itikija amesema wilaya ya Hai inaendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na takwimu za kimkoa na kitaifa, ambapo kiwango cha udumavu ni asilimia 13, ikilinganishwa na asilimia 20 ya mkoa wa Kilimanjaro na asilimia 31 kwa Taifa zima.

Amesema licha ya mafanikio hayo, bado juhudi zinaendelea kuhakikisha wananchi wote wanapata lishe bora na kupunguza zaidi changamoto ya udumavu.

Sauti ya Dr itikija msuya akizungumza baada ya kikao cha lishe

Kwa upande wake Afisa Lishe wa Wilaya ya Hai, Abel Mwaipungu amesema tathmini ya lishe hususan katika shule za wilaya hiyo inaonesha hali ni nzuri, huku serikali ikiendelea kuhakikisha shule zote zinapatiwa unga wa lishe ulioongezwa virutubisho.

Sauti ya Afisa Lishe Wilaya ya Hai Abel Mwaipungu akizungumza baada ya kikao cha Lishe
Pichani ni wataalamu wa Lishe na maafisa watendaji wa wilaya ya Hai

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Hai, Hassan Bomboko amewataka watendaji wa kata zote 17 kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi na shule zote kwa wakati, pamoja na kutoa taarifa za lishe kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe. Hassan Bomboko akizungumza wakati wa kikao cha Lishe

Aidha Bomboko amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti za gharama na upatikanaji wa vifaa vinavyotumika katika uzalishaji wa lishe bora katika ngazi ya kata.