Boma Hai FM
Boma Hai FM
2 February 2026, 6:59 pm

Katika kuadhimisha miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi, kata ya Masama Kati imepanda miti katika kituo cha Afya Masama kati pamoja na kutembelea jengo la wamama wajawazito na kuwalipia gharama za matibabu.
Na Oliver Joel, Hai-Kilimanjaro
Katika kuadhimisha miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) leo 2 febr 2025,wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata matibabu katika kituo cha afya cha Masama Kati ambacho kwa sasa serikali imeboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali.
Wito huo umetolewa na diwani wa kata ya Masama kusini Kandata Kimaro
alipokuwa kituoni hapo wakati akizungumza na wagonjwa waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu na kuahidi kulipia gharama zao za matibabu,ikiwa ni katika kuadhimisha miaka 49 ya chama hicho.
Katika maadhimisho hayo yaliyoambatana na zoezi la upandaji miti, mheshimiwa Kimaro amesema kuwa lengo la kupanda miti ni kutunza mazingira ya eneo hilo kwa manufaa ya sasa na baadae.
Naye mwenyekiti wa chama cha mapinduzi kata ya Masama Kati Josephat Ndosi amemshukuru mbunge wa Hai kwa jinsi alivyojitoa kwa ajili ya kuhakikisha fedha za mradi huo zinafika kwa wakati ,ambapo ameongeza kuwa upandaji miti uliofanyika katika kituo hicho ni kuenzi juhudi kubwa zilizofanywa na waasisi wa chama hicho.

Mwenyekiti wa kijiji cha Lemira Kati kilichopo katika kata hiyo Jefta Silaa amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha afya umekuwa na maanufaa kwa wananchi kwani kwa sasa wanapata huduma ya matibabu ndani ya kata yao kwani hapo awali walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata matibabu.
Naye mmoja wa wananchi waliofika katika kituo hicho Gilbert Ezekia na Catherine Robert wameelezea namna walivyofurahia uwepo wa kituo hicho ambacho kimekuwa mkombozi kwao huku wakiwasihi wananchi wengine kufika kituoni hapo kwa ajili ya matibabu badala ya kufuata huduma hiyo katika vituo vingine.
Naye mganga mfawidhi wa kituo cha afya Masama Kati amesema kuwa kwa sasa kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali huku wazee na watoto pamoja na wajawazito wakipata huduma bila malipo.